Jengeni maisha yenu katika ukweli, utakatifu, furaha na kweli za Kiinjili!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa, tarehe 2 Mei 2014 ameadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wajumbe wa Chama cha Vijana Wakatoliki waliokuwa
wanashiriki mkutano mkuu wa kitaifa uliofanyika mjini Roma. Katika mahubiri yake anasema,
hata yeye amekuwa ni mkereketwa na mwanachama hodari, mambo ambayo yameacha chapa
ya kudumu katika maisha na utume wake. Amekuwa karibu na chama cha vijana Wakatoliki
kwa njia ya sala!
Kardinali Parolin anawataka vijana wakatoliki kuwa watu wapya
wanaoongozwa na mwanga wa Neno la Mungu na Mafundisho ya viongozi wa Kanisa, ili kujenga
msingi thabiti kwa maisha ya baadaye. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina unaopaswa
kuendelezwa majimboni na parokiani, ili kuleta matumaini mapya. Vijana kwa njia ya
ushuhuda wa maisha yao wanasukumwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka, yaani
mateso, kifo na ufufuko wa Yesu.
Vijana wanapaswa kuwa waaminifu kwa Kristo
na Kanisa lake kwa kutekekeza nyajibu zao kwa weledi na umakini mkubwa, huku wakiendelea
kupata majiundo ya maisha na wito wa Kikristo katika maisha ya kiutu, kifamilia, kikazi
na kisiasa. Ni mwaliko na changamoto ya kushikamana kidugu na maskini pamoja na kusimama
kidete kupinga vitendo vyote vinavyosababisha uvunjifu wa haki.
Lengo kama
anavyosema Baba Mtakatifu ni kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni mwa jamii kwa kukazia
mambo msingi katika maisha. Vijana waendelee kushirikiana na kuwajibika pamoja na
viongozi wao wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo. Hakuna
haj aya kukata tamaa kutokana na mapungufu ya rasilimali na uwezo wa kukabiliana na
matatizo pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha; kama vile
ukosefu wa fursa za ajira, magonjwa, vita, madhulumu na nyanyaso mbali mbali, bali
kila mtu atekeleze wajibu wake kikamilifu, ili kuwasha tena cheche za matumaini kwa
wale waliokata tamaa!
Kardinali Pietro Parolin anawataka vijana wakatoliki
Italia kuendelea kuenzi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao mifano na mafundisho ya
Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II kwa kujikita katika ukweli, utakatifu wa
maisha na furaha ya kweli; imani kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kujikita katika
kweli za Kiinjili.