2014-05-02 08:55:28

Wananchi wa Zambia wanahitaji Katiba Mpya!


Baraza la Makanisa Zambia, CCZ hivi karibuni katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, limesikitishwa na vitisho vilivyotolewa na Rais Michael Chilufya Sata wa Zambia dhidi ya Askofu George Lungu wa Jimbo Katoliki Chipata, baada ya kusali Jimboni kwake kwa ajili ya kuiombea Serikali ya Zambia iweze kuwapatia wananchi Katiba mpya.

Baraza la Makanisa Zambia linasema, vistisho hivi haviwezi kukubalika kamwe, kwani wananchi wa Zambia wanahitaji Katiba Mpya ambayo imekuwa ikipigwa dana dana na viongozi mbali mbali wa Serikali wanapoingia madarakani. Baraza la Makanisa linasema katika taarifa yake kwamba, Makanisa hayawezi kukaa kimya na kuwaona wananchi wa Zambia wakiendelea kuogelea katika umaskini, ujinga na maradhi, huku watu wachache wakiendelea kufaidika na rasilimali za nchi kutokana na ukosefu wa wa utawala bora.

Katiba Mpya nchini Zambia ni hitaji msingi na kamwe Makanisa hayatakaa kimya, hadi pale wale waliopewa dhamana na madaraka ya kuwaongoza wananchi wa Zambia watakapotekeleza wajibu wao na kwamba, kuomba Katiba Mpya si kwamba Kanisa linataka kuingilia mambo ya kisiasa, bali linatekeleza sauti yake ya kinabii kwa wananchi wasiokuwa na sauti! Watu ambao wanataka kunyamazishwa na wenye madaraka serikalini.

Baraza la Makanisa Zambia linamwomba, Rais Michael Sata kuwapatia wananchi wa Zambia Katiba Mpya bila kuchelewa kabla mambo hayajaharibika.







All the contents on this site are copyrighted ©.