Uwajibikaji wa binadamu katika kudumisha mazingira endelevu!
Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii
kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Mei, 2014, zinaendesha Warsha ya pamoja inayojadili
pamoja na mambo mengine kuhusu binadamu anavyoendeleza utunzaji wa mazingira asilia
kwa ajili ya mafao yake kwa sasa na kwa vizazi vijavyo; kwa kuibua na kubuni mikakati
na sera za uchumi endelevu; pamoja na matumizi sahihi ya ujuzi na maarifa.
Hii
inatokana na ukweli kwamba, mwanadamu anahitaji mazingira bora kwa ajili ya ustawi
na maendeleo yake, lakini takwimu zinaonesha kwamba, mwanadamu amekuwa pia ni chanzo
kikuu cha uharibifu wa mazingira kutokana na matumizi mabaya ya rasilimali ardhi.
Binadamu anapaswa kubadili tabia na mwenendo wake wa maisha. Kumekuwepo na ongezeko
kubwa la mahitaji ya chakula duniani, watu wanaishi kwa muda mrefu zaidi na hali ya
uchumi kwa mataifa mengi imeboreka kwa kiasi kikubwa, lakini tatizo la uharibifu mkubwa
wa mazingira kwa sasa na kwa siku za usoni kati ya changamoto kubwa ambazo Jumuiya
ya Kimataifa inapaswa kuzikabilia.
Kuna baadhi ya watu wanahusisha ukuaji wa
uchumi na uchafuzi wa mazingira na kwamba, baadhi ya wataalam wanapenda kugusia suala
la mikakati ya maendeleo endelevu, wanapozungumzia ukuaji wa uchumi kimataifa, pengine
na kusahau kuangalia changamoto za ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea duniani.
Lakini ikumbukwe kwamba, uchafuzi wa mazingira unaosababisha athari kubwa za mabadiliko
ya tabia nchi ni chanzo kikubwa cha majanga kwa nchi tajiri na maskini duniani.
Kukua
na kukomaa kwa uchumi katika nchi tajiri katika sekta ya viwanda na kilimo, kumechangia
kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira duniani na kwamba, hadi sasa hakuna sera makini
zilizokwisha ibuliwa ili kudhibiti hali kama hii, kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya wengi. Brazil, Russia, India, China na Afrika ya Kusini, BRICS kama zinavyotambuliwa
na wengi zinaendelea kufuata mkondo huo huo wa uchafuzi wa mazingira kiasi cha kuhatarisha
maisha ya viumbe hai kwa siku za usoni.
Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya
watu duniani inaendelea kuongezeka maradufu, kiasi kwamba hata mahitaji ya nishati
yanaongeza kwa kasi ya ajabu; mambo yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa uharibu
wa mazingira. Kupanuka kwa kiwango cha elimu na ufahamu wa masuala ya kisayansi, uwekezaji
katika miundo mbinu, ubora wa elimu ya juu na ukuaji wa viwanda ni kielelezo kwamba
watu wengi wamekuwa na ufahamu mkubwa wa madhara ya uchafuzi wa mazingira katika Nchi
tajiri zaidi duniani ikilinganishwa na watu wanaoishi katika nchi maskini.
Taasisi
za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii zinasema kwamba, dhamana na uwajibikaji wa kimaadili
ni muhimu sana, ingawa ni jambo ambalo halijapewa msukumo wa kutosha. Kuna haja ya
kufanya mabadiliko yanayolenga kuleta maboresho katika uhusiano kati ya binadamu na
mazingira, ili kuibua na kuimarisha mikakati itakayosaidia kuendeleza sera na mipango
endelevu ya kiuchumi na maendeleo jamii.
Mkutano wa Kimataifa katika kudhibiti
madhara ya mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mjini Rio de Janairo, ulishindwa kufikia
malengo yake kutokana na misigano mikubwa iliyojionesha kati ya wajumbe waliokuwa
wanahudhuria. Wajumbe wa Taasisi za Kipapa za Sayansi na Sayansi Jamii zinataka kuhimiza
ubinadamu endelevu kwa ajili ya kuenzi mazingira bora, kwa kutambua kwamba, mwanadamu
na mazingira ni mambo yanayotegemeana katika: mahitaji, chakula, afya na nishati.
Watalaam kutoka katika medani za sayansi na sayansi jamii wakishirikiana kwa dhati
wanaweza kuleta uhusiano mwema kati ya binadamu na mazingira yake.