2014-05-02 07:43:49

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Pasaka


Mpendwa mwana wa Mungu ninakuleteeni tena furaha ya Pasaka kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu tukiwa tayari Dominika ya tatu ya Pasaka. Ujumbe wa Neno la Mungu Dominika hii ni ule usemao, "Wakamtambua katika kuumega Mkate". Katika somo la kwanza toka Kitabu cha Matendo ya Mitume tunapata kukutana na sehemu ya mahubiri ya Mtakatifu Petro. RealAudioMP3

Katika mahubiri haya Mtakatifu Petro akiwa amejawa na Roho wa Mungu na nguvu ya Pasaka anatangaza kuwa Kristu aliyedhihirishwa kwetu na Mungu na kuteswa na kisha kutundikwa msalabani, amefufuliwa na Mungu. Jambo hili ni la kweli na hakika, kwa maana sisi tu mashahidi. Mtakatifu Petro anashuhudia hilo akisema tulikula, na tukanywa pamoja naye na si hilo tu bali tumeshuhudia na kufuata mafundisho yake hadi anapofufuka.

Mpendwa msikilizaji, Mtakatifu Petro analenga kufundisha na kusimika imani katika Bwana mfufuka na tokea pale kuweza kusonga mbele katika utume kadiri Bwana alivyoagiza.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mtakatifu Petro anasonga mbele akijaribu kuweka wazi mpango wa Mungu uliojificha katika kifo cha Bwana. Anakazia na anasema ni kweli kifo chake kilikuwa ni sehemu ya mpango wa Mungu. Katika hoja hii anajaribu kujibu maswali ya wale walioona kifo cha Kristu kama kikwazo na hasa wanapofikiri na kutambua kuwa yeye alikuwa Masiha! Anasema kile kinachoonekana kwetu kama makwazo na madhulumu kwa Mungu ni ishara ya ushindi! Kwa njia ya kifo kuna maisha mapya, yaani maisha ya ufufuko.

Katika somo II toka barua ya Mt Petro, (1Pet. 1:17-21) tunakutana na mwendelezo wa mafundisho juu ya ubatizo. Anawaambia wabatizwa wapya kwamba sasa wanao uwezo na nguvu za kumwita Mungu “Baba” kwa sababu wamepokea maisha mapya toka yeye. Ni zawadi kubwa na nono lakini pia inayo sehemu ya wajibu mkubwa nao ni kuwa mpya na daima kukaa katika hali ya utu upya! Mtakatifu Petro anasonga mbele akisema kwa kupata zawadi ya ubatizo na yote yaambatanayo na zawadi hiyo, mfano kumwita Mungu “Abba” kunatupasa kutambua kuwa kuna mmoja ambaye amelipia fidia.

Ndiyo kusema si kwa fedha wala dhahabu bali kwa DAMU YA MWANA WA MUNGU!, Damu ya Kristu mpakwa mafuta wa Bwana! Damu isiyo na doa la dhambi. Kumbe tumekombolewa kwa Damu ya thamani kuu mno! Yule kondoo ambaye Waisraeli walikuwa wakimchinja wakati wa sherehe za Pasaka ilikuwa ni kiashilio cha Kristu kondoo wa AJ ambaye anajitoa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.

Katika somo III toka Mwinjili Luk 24:13-35, tunapata simulizi la wanafunzi 2 wa Emmaus. Mmoja wa wanafunzi hawa anaitwa Kleopa na mwingine jina lake halijulikani. Habari njema imewekwa katika mtindo wa katekesi, Ni Kristu mfufuka anafundisha watu wake na ndio sisi wenyewe na mafundisho ni juu ya ufufuko wake. Mwinjili Luka anamtaja mwanafunzi mmojawapo kuwa Kleopa ambaye kadiri ya tafiti za kibiblia alikuwa ni kaka yake na Yosefu, baba yake mlishi wa Yesu Kristu yaani Bwana.

Mwingine hatajwi jina, Luka akitaka kuacha nafasi kwa ajili yetu sisi ambao tunaalikwa kufuata nyayo zake tukimwelekea Bwana Mfufuka. Hawa wanafunzi wanakimbia toka Yerusalemu kwa maana matarajio yao hayakutimia. Walitarajia Masiha mshindi, mwenye nguvu, na mwenye kuishi maisha marefu na badala yake wanamwona akishindwa na kufa akiwa na miaka 33!.

Mpendwa msikilizaji, ndugu hawa wakiwa katika majadiliano ghafla Bwana ataingilia majadiliano yao na kuwauliza mnajadiliana nini? Hawa wanafunzi wawili wanasimama na kukasilika wakishangaa mtu huyu ni nani asiyejua kilichotokea Yerusalemu? Atawauliza tena kwani kumetokea nini?

Basi wanafunzi hawa watahadithia habari za Yesu Mnazareti jinsi alivyokuwa na uwezo mkuu lakini wakuu wa walimtia nguvuni na kumsulubisha! Wanafunzi hawa wanasema kwa kweli hatuoni tumaini tena na ndiyo maana tunakimbia! Mara kadhaa hata sisi tunalo tumaini fulani katika maisha, lakini inapojitokeza hatufaulu basi ni kuanza kulalamika na kukata tamaa kama ndugu hawa na hata wengine kuliacha Kanisa.

Angalia hali ya kisiasa kunakuwa na tumaini fulani kwa watu fulani na wanaponyamazishwa basi matumaini yetu huanguka pia! Hata hivyo mpendwa unayenisikiliza, mkristu anayeamini katika ufufuko hawezi kukatishwa tamaa na mikasa inayojitokeza katika maisha bali anasonga mbele kama Kristu mpaka Kalvari ambapo ndipo kuna ufufuko!

Mpendwa katika Bwana, wanafunzi wa Emmaus walikuwa na ujuzi juu ya Bwana lakini ujuzi wao uliishia katika kifo cha Bwana tu, hawakuweza kuendelea mbele! Hawakutambua kuwa Bwana alikuwa amefufuka na hiki ndicho kisa cha kukata tamaa, maana kama ni kifo tu, kwa hakika kinatisha na kukatisha tamaa. Ndiyo kusema nasi wakati fulani tunapoanza safari ya kumtafuta Bwana tunaishia kwenye kifo pasipo kwenda mpaka ufufuko na hapa ndo kuna taabu na mikato ya tamaa isiyohesabika! Tunaalikwa kwenda mbele mpaka ufufuko.

Hatupaswi kuishia katika kumwona Bwana kama mwana mapinduzi bali kama mwokozi wetu. Tunaalikwa kwenda mpaka ufufuko ambao huwezi kuufafanua kwa mahesabu bali kwa imani na hapa ndipo kuna hekima ya Kimungu. Wanafunzi wa Emmaus wana huzuni kwanza kuacha jumuiya yao ambamo wangeweza kupata majibu ya wasiwasi wao.

Shida nyingine hawakutaka kufanya utafiti juu Ya kile kilichosemwa na akina mama waliokwenda makaburini siku ya ufufuko. Pengine waliona kwa kuwa kimahesabu haiwezekani kukifafanua na hivi wanazama katika dharau na hili ni ukosefu wa imani! Leo hii katika Jumuiya yetu ya Kanisa kuna watu ambao kukitokea shida kidogo ni kuanza kukimbia wakifikiria wataweza kupata majibu na badala yake ni kukumbana na mkato wa tamaa na udhaifu wa kiroho kukua na kuongezeka. Fundisho katika hili ni kwamba yafaa siku zote kukaa na jumuiya na kutafuta suluhisho la matatizo yetu na ya Kanisa ndani ya Jumuiya yetu.

Mpendwa katika Bwana pamoja na kwamba ndugu hawa wawili wamekata tamaa na wanaujuzi nusunusu juu ya Bwana, Bwana hawaachi anaambatana nao na kuwasaidia polepole ili waweze kuelewa nini kilitokea na kwa nini ilikuwa vile. Hata kwetu hivi leo Bwana anatupa company tunapokuwa katika hali ya kukimbia matatizo na kukata tamaa. Ndiyo kusema nasi tuwape company kaka na dada zetu wakiwa katika taabu.

Mpendwa msikilizaji, ndugu hawa pamoja na kwamba Bwana amewasaidia katika shida yao ya kutoelewa vema maandiko matakatifu bado wanamwona kama msafiri mwenzao, mwenye shida kama wao. Mpendwa yatupasa kukazia lengo letu katika maisha, maana yake tukilipoteza hata mmoja anapojaribu kutueleza akili haipokei haraka.

Katika shida kama hii Bwana atafanyaje? Kwa hakika anaanza kuwafafanulia maandiko matakatifu kuanzia AK mpaka AJ linalomhusu yeye mwenyewe na hasa juu ya mateso hadi ufufuko wake. Ndiyo kusema Kwa njia ya Neno la Mungu mtu huweza kutambua mafumbo ya Mungu. Hata hivyo pamoja na hilo hawakuweza kuelewa kitu na Bwana atawakemea kwa mioyo migumu hiyo. Kwa hakika hata hivi leo shida ya kutoelewa na hasa kutoguswa na Neno la Mungu ipo, yafaa kuomba sana nguvu ya Roho Mtakatifu kwa ajili hiyo.

Mpendwa Bwana akiendelea na katekesi yake inafika jioni na anataka kuendelea mbele wakati wanafunzi wamefika. Basi wanamkaribisha nyumbani walipokuwa wanaenda na kisha ataketi chakulani pamoja nao na KUUMEGA MKATE na kuwapatia. Kwa tendo la kuumega mkate macho yalifunguka na wakamtambua kuwa ni BWANA MFUFUKA na mara atatoweka! Swali linawajia kwa nini hatukumtambua alipokuwa anatufafanulia Maandiko Matakatifu? Basi mara moja ndugu hawa walirudi Yerusalemu kwa furaha bila wasiwasi tena na kutangaza habari njema wakisema tumemwona Bwana mfufuka na kweli amefufuka.

Mpendwa katika Bwana simulizi la wanafunzi wa Emmaus kadiri ya Mt. Yustini ni chimbuko la mpango wa Misa Takatifu. Waamini kuingia mapema katika ibada, hii ni sawa na wanafunzi wa Emmaus kuwa njiani tokea Yerusalemu, kuingia kwa Padre kwa maandamano ni ishara ya kuingia kwa Kristu masiha katika majadiliano ya wanafunzi hawa. Mahubiri ni ishara ya ufafanuzi wa Neno la Mungu uliofanywa na Bwana mfufuka na Litrujia ya Ekaristi Takatifu yaturudisha katika ishara ya Kristu kuumega mkate na kuwapa wanafunzi wa Emmaus.

Mwishoni mwa Misa Padre huondoka kwa maandamano toka kwenye Misa kabla ya waamini wengine, hii yaturudisha katika lile tendo la Bwana kutoweka mara baada ya kumega mkate na kuwapatia. Wanafunzi wa Emmaus walipoelewa haya, walirudi Yerusalemu wa furaha kutangaza furaha ya ufufuko. Mpendwa, wewe je baada ya kuumega mkate waondoka katika Misa kwa furaha kwa ajili ya kutangaza kwa wengine au warudi nyumbani kwa huzuni? Tafakari hili!
Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, nawe ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya ukienda kutangaza habari ya ufufuko wa Bwana kwa furaha kuu. Tukutane tena Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.