2014-05-02 14:10:01

Rasilimali ya Kanisa itumike kwa kuzingatia ukweli na uwazi!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa wajumbe wa Baraza la Kipapa la Uchumi alililoanzisha hivi karibuni anasema kwamba, anapenda kuona Kanisa linatekeleza dhamana yake kwa kuwajibika pamoja na kuwa na matumizi bora ya rasilimali yake yanayoongozwa katika misingi ya ukweli na uwazi mintarafu kazi ya uinjilishaji, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Vatican inapaswa kutekeleza dhamana hii kwa kukazia misingi hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu. Zote hizi ni juhudi za mabadiliko ya kina kwa ajili ya kufanya maboresho katika Sekretarieti ya Vatican, ili kutoa huduma bora na makini kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu, changamoto na mwaliko kwa sekta mbali mbali kuanza kuwa na mwelekeo mpya zaidi kwa kuwa makini katika kusimamia na kutumia rasilimali ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, tume hii inafanya kazi zake kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti ya uchumi. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwatakia kheri na baraka wajumbe wote katika utekelezaji wa dhamana hii nyeti na kwamba, Baraza hili linawakilishwa na wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuchangia katika uzoefu na mang'amuzi kwa ajili ya huduma ya Kanisa. Wajumbe walei wana haki sawa kabisa na wala hakuna upendeleo.







All the contents on this site are copyrighted ©.