2014-05-02 07:51:18

Mtakatifu Yohane XXIII ni Baba wa majadiliano ya kiekumene!


Askofu mkuu Gennadios wa Kanisa la Kiorthodox nchini Italia na Malta anamshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo aliyemwezesha Baba Mtakatifu Francisko kuwatangaza na hatimaye Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuandikwa kwenye orodha ya watakatifu, katika Ibada ya Misa takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. RealAudioMP3

Mtakatifu Yohane XXIII ni kiongozi aliyepata uzoefu na mang’amuzi makubwa wakati alipokuwa anatekeleza utume wake kama Mwakilishi na Balozi wa Vatican nchini Bulgaria na Uturuki, akabahatika kuwa kweli ni daraja na kiungo muhimu kati ya Mashariki na Magharibi.

Ni Baba na muasisi wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, alionesha dira na mwongozo kwa Kanisa Katoliki kwa kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Wakristo, ili wote waweze kuwa wamoja kadiri ya sala na matashi ya Kristo mwenyewe. Alikuwa ni kiongozi, mwema na mpole, aliyesheheni unyenyekevu na utu wema; alikuwa ni mpenda amani na mapatano kati ya watu; akapenda na kuthamini maisha na tunu msingi za kifamilia; aliwajali na kuwapenda maskini na wote waliokuwa wanateseka kutokana na hali ngumu ya maisha; kiasi cha kupendwa na wengi.

Kwa maneno machache, Mtakatifu Yohane XXIII anaweza kwa uhakika kuitwa kuwa ni Baba wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa, aliyeweka msingi thabiti katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kwa sasa na kwa siku za usoni!

Mtakatifu Yohane XXIII anakumbukwa na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox kama kiongozi aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, zote hizi anasema Askofu mkuu Gennadios kwamba, ni cheche za utakatifu wa maisha zilizooneshwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa Katoliki na ulimwengu katika ujumla wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.