Mfuko wa Kipapa umechangia maendeleo ya watu duniani!
Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza wajumbe wa Mfuko wa Papa waliomtembelea mjini
Vatican, Ijumaa tarehe 2 Mei 2014, wakati huu Wakristo sehemu mbali mbali za dunia
wanapoendelea kusherehekea ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na kifo pamoja na kupokea
zawadi ya Roho Mtakatifu anayefanya yote kuwa mapya.
Baba Mtakatifu anawaombea
furaha na amani ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo mfufuka na kwamba, hija ya
sala katika Makaburi ya Watakatifu na wafiadini viwawezeshe kuendelea kuwa waaminifu
kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anasema, tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Kipapa,
umesaidia kugharimia utume na maisha ya Kanisa kwa njia ya matendo ya huruma kadiri
ya nia za Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa
Mfuko wa Kipapa kwa mchango wao katika maendeleo na ustawi wa Kanisa katika nchi zinazoendelea
duniani. Mchango huu umekuwa ni msaada mkubwa katika huduma kwenye sekta ya elimu,
miradi ya huduma, pamoja na kusaidia kugharimia majiundo kwa waamini walei, watawa
na mapadre wanaosoma mjini Roma.
Kwa njia hii, Mfuko wa Kipapa umekuwa mstari
wa mbele katika kunoa akili na mioyo ya vijana wa kizazi kipya kadiri ya kweli za
Kiinjili na hekima inayobubujika kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kukazia
umoja na mshikamano ndani ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa binadamu wote.
Baba
Mtakatifu anawatakia kheri na mafanikio mema, ili waendelee kuimarishwa katika neema
ya ubatizo inayowasukuma kuwa kweli ni wamissionari wa Habari Njema ya Wokovu, wakati
huu Mama Kanisa anapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa watakatifu
Yohane XXIII na Yohane Paulo II, ili wanapokutana na Yesu Mfufuka awe kweli ni chemchemi
ya furaha yao ya ndani.