2014-05-02 10:12:33

Jubilee ya Miaka 100 ya Kanisa kuu la Mtakatifu Augustino, Algeria


Kanisa Katoliki nchini Algeria linaadhimisha Jubilee ya Karne Moja tangu Kanisa la Mtakatifu Augustino lilipopandishwa hadhi na kuwa ni Kanisa kuu, ambalo hivi karibuni, limefanyiwa ukarabati mkubwa. Maadhimisho ya Jubilee hii yameanza kutimua vumbi tarehe 2 Mei 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, kama mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu Francisko.

Ukarabati wa Kanisa hili umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ufadhili kutoka ndani na nje ya Algeria. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amechangia kwa kiasi kikubwa katika ufadhili huo. Akizungumzia kuhusu tukio hili Askofu Paul Desfarges wa Jimbo Katoliki Costantina, Algeria anasema kwamba, Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anawachangamotisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwendea Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, kwani anawasubiri, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Mtakatifu Augustino ni kielelezo cha watu wanaotafuta ukweli na maana katika maisha, ili hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu.

Kardinali Jean Luis Tauran anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza Wakristo na Waislam kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kujenga misingi ya haki, amani, usawa na mshikamano wa kitaifa. Maisha na kazi zilizofanywa na Mtakatifu Augustino ziwasaidie waamini kutambua kwamba, hakuna ukinzani kati ya imani na uwezo wa mtu kufikiri na kutenda.

Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia moja ya Kanisa la Mtaakatifu Augustino yawe ni changamoto kwa waamini kuendelea na hija ya kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yao; wakiendelea kuwa waaminifu kwake na kwa Kanisa lake. Wajenge na kudumisha moyo wa ibada na sala; kwa tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma.

Majadiliano ya kidini yajengeke na kusimikwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida, kwa kudumisha udugu na urafiki; kwa kufahamiana na kupendana. Dini mbali mbali duniani zinapaswa kuwa ni chemchemi ya amani, umoja na udugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.