Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II walikuwa ni watetezi wa wafanyakazi!
Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu mfanyakazi kwa Mwaka 2014 yanatajirishwa
kwa namna ya pekee na uzoefu pamoja na mafundisho ya kina yaliyotolewa na Watakatifu
Yohane XXIII na Yohane Paulo II, waliosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Hawa ni watakatifu waliotangazwa
na Papa Francisko hivi karibuni hapa mjini Vatican.
Watakatifu hawa wameshuhudia
mateso na mahangaiko ya wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia enzi ya maisha
na utumishi wao kama Mapadre, Maaskofu na baadaye kama Mapapa. Hawakukata tamaa kuonesha
umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu kwa njia ya
ushuhuda wa maisha yao wenyewe!
Ni ujumbe kutoka kwa Askofu mkuu Cesare Nosiglia
wa Jimbo kuu la Torino, Italia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Anasema, kuna haja ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika
kujenga, kulinda na kudumisha misingi ya haki katika maeneo ya kazi, ili kuamsha tena
matumaini miongoni mwa wafanyakazi wanaoendelea kukata tamaa ya maisha bora kutokana
na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Askofu mkuu Nosiglia anawataka wafanyabiashara
kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji mali na utoaji wa huduma, kama sehemu
ya mchakato wa kutengeneza fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana. Juhudi hizi hazina
budi kwenda sanjari na urahisishaji wa huduma kwa kuondokana na ukiritimba usiokuwa
na mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wananchi.
Anawataka vijana kujenga matumaini
kwa kuwekeza katika karama na vipaji walivyokirimiwa na Roho Mtakatifu ili kutengeneza
fursa za ajira, kwa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja, mwanadamu akipewa kipaumbele
cha kwanza kabisa.
Vyama vya wafanyakazi, vishikamane kulinda na kutetea masilahi
ya wafanyakazi, washirikiane na wafanyakazi pamoja na waajiri wao, ili kuleta tija
na ufanisi mkubwa katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwa jamii. Kuna haja ya kuwekeza
katika mafunzo kazini, kwa kuthamini tunu msingi za maisha ya kifamilia pamoja na
kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto katika ulimwengu wa wafanyakazi kwa busara!
Wafanyakazi
wajenge imani kwa Mungu na binadamu, waongeze mtazamo wao katika masuala ya kiulimwengu
na kamwe wasijitafute wenyewe katika ubinafsi wao, kwani watajikuta wakitumbukia katika
umaskini si tu wa kiuchumi bali hata pia umaskini wa kitamaduni. Woga na wasi wasi,
hasira na chuki ni mambo yasiyokuwa na maendeleo katika shughuli za uzalishaji na
utoaji wa huduma.
Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, anawataka
wafanyakazi kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Kanisa linakiri
na kufundisha juu ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akawa sawa na binadamu, akafanya
kazi, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na hivyo kufanya yote mapya!
Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi na Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II
waendelee kuwaombea wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia ili watambue kwamba, kazi
ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu inayomshikirisha pia katika kazi ya uumbaji
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii inayowazunguka!