2014-05-01 07:08:35

Ni ruksa kutembelea Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameridhia wazo la kufungua milango kwa Jamii kutembelea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo na viunga vyake, iliyojengwa kunako tarehe 10 Mei 1626 wakati Papa Urbano wa VIII alipoanza kutumia Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo kama makazi ya Kipapa wakati wa kiangazi. Haya ni makazi ambayo yamekuwa pia ni kimbilio la watu wengi wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, Papa Pio wa XII alipotoa hifadhi kwa wakimbizi waliokuwa wanatafuta njia ya kuhifadhi maisha yao. RealAudioMP3

Hivi ndivyo anavyosimulia Dr Osvaldo Gianol aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa ni Msimamizi mkuu wa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, kwa kutoa mwaliko kwa watalii wa ndani na nje ya Italia kutembelea Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo ili kujionea wenyewe maajabu ya Mungu kwa njia ya mikono ya wanadamu. Watalii watapata fursa ya kutembelea pia Bustani zilizoko Castel Gandolfo pamoja na kupata maelezo ya kina yanayogusa historia na umuhimu wake.

Akizungumzia kuhusu jitihada hizi, Dr Antonio Paolucci, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Vatican anasema, ndani ya Bustani ya Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, watalii wataweza kuona mambo mengi ya kihistoria, sehemu ya mapumziko na mahali pa kuvulia samaki, kwani Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo imejengwa kwenye ukingo wa Ziwa. Samaki wanaovuliwa ziwani humo wakati wa majira ya kiangazi ni kwa jili ya kusaidia watu wenye shida mbali mbali.

Matembezi kwenye Bustani za Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo yanaweza kufanyika kwa muda wa saa nzima na yataendelea kusimamiwa na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Vatican, ambaye bado “anakuna kichwa” ili kuweka bayana mikakati iitakayowawezesha watalii kufaidika na matembezi watakayofanya ndani ya Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Matembezi haya yamefunguliwa rasmi hapo tarehe Mosi Machi 2014.

Kwa sasa watalii hawataweza kutembelea ndani ya vyumba vya Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo kwani hii ni ziara inayohitaji mikakati makini ya ulinzi na usalama. Matokeo ya sasa yatasaidia kuweka mikakati kwa siku za usoni. Wafanyakazi wa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo wamepokea wazo hii kwa furaha kwani ni fursa itakayowawezesha kutumia weledi wao kwa mapana zaidi.

Wananchi wa Castel Gandolfo wanafurahia kwa sababu mbali mbali hasa zaidi kwa kukuza na kuendeleza utalii katika eneo hili. Uongozi wa Makumbusho ya Vatican unawahimiza watalii kufanya ziara za makundi ili kupata watu watakaowaongoza na kuwaelekeza.








All the contents on this site are copyrighted ©.