Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi ni fursa inayotolewa na Jumuiya
ya Kimataifa kila mwaka kwa wafanyakazi kufanya tathmini ya kina kuhusu kazi walizotenda,
ufanisi na tija katika shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma pamoja na kujiwekea
malengo kwa siku za usoni kwa kukazia umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau mbali mbali
katika kazi.
Katika mazingira ya utandawazi usiojali mateso na mahangaiko ya
watu, kuna haja ya kuanzisha na kuimarisha mshikamano wa kidugu unaojengeka katika
vyama vya ushirika miongoni mwa wafanyakazi, kwa kutambua na kuendelea kudumisha sheria,
kanuni na usalama kazini. Mishahara mizuri, mazingira safi na bora ya kazi pamoja
na vitendea kazi vizuri ni mambo ambayo yanaweza kuchangia katika maboresho na ufanisi
kazini sanjari na ukuzaji wa pato la wafanyakazi.
Ubadhirifu wa mali ya umma,
ufisadi, wizi na hujuma kazini ni mambo ambayo daima yamekwamisha ufanisi kazini na
matokeo yake ni watu kuendelea kukomaa katika ubinafsi na utandawazi wa kutojali wala
kuguswa na mahangaiko ya jirani. Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani, iwe ni fursa ya
kukuza na kuimarisha sheria za kazi, utawala bora na usalama kazini.
Siku kuu
ya Wafanyakazi imewekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Siku kuu hii
ndani ya Kanisa ilianzishwa kunako mwak 1955 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili.
Lengo ni kutambua heshim ya kufanya kazi kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima
ya binadamu. Huu ni mwendelezo wa kuutiisha ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Watu wanapaswa kutambua kwamba, kazi ni sehemu muhimu sana katika
maisha ya mwanadamu kwani ni sehemu ya ubinadamu na matokeo ya kazi.
Utu na
heshima ya mwanadamu ndicho kipimo sahihi cha heshima ya kazi. Kazi ni wajibu na utambulisho
mwa wanadamu na kwamba, nguvu kazi ina kipaumbele cha kiasili zaidi ya mtaji, kumbe,
kuna haja ya kuwa na uhusiano unaokamilishana kati ya kazi na mtaji, lakini utu na
heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.