2014-05-01 07:54:53

Fedha ikithaminiwa sana, uwepo wa Mungu na utu wa mwanadamu vinawekwa rehani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa mwaka 2014 linasema kwamba, pale jamii inaposhindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na uwepo wa Mungu na badala yake fedha na mali vinapewa msukumo wa pekee, hapo kuna hatari ya kuibuka kwa misigano ndani ya Jamii na hivyo kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu unaogusa mahitaji ya mtu kiroho na kimwili.

Maaskofu wanaendelea kusema kwamba, pale fursa za ajira zinapokosekana, utu na heshima ya mwanadamu vinawekwa rehani. Ukosefu wa fursa za ajira, mazingira duni ya kazi, athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kazi za suluba zinazofanywa na watoto, ubaguzi wa rangi na ukosefu wa usawa katika utoaji wa mishahara pamoja na mazingira mabaya ya kazi ni mambo ambayo yanasababisha madonda makubwa katika utu na heshima ya wafanyakazi, kiasi kwamba, athari zake pia zinajionesha kwenye familia kwa kushindwa kutekeleza nyajibu zake barabara.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika kwa namna ya pekee waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na wafanyakazi wanaokumbana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kiasi kwamba hawana tena matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.

Maaskofu wanawakumbuka wafanyakazi waliopoteza maisha yao wakiwa wanatoa huduma kwa jamii, matukio ambao kimsingi yanasababishwa na ukosefu wa usalama kazini na maelezo ya kina. Vifo na ajali kazini ni matukio ambayo yanaacha madonda makubwa kwa familia za wafanyakazi na taifa katika ujumla wake, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, usalama kazini unapewa pia kipaumbele cha kutosha.

Vyama vya wafanyakazi visipotekeleza dhamana na wajibu wake, wafanyakazi wataendelea kupoteza maisha, kupata vilema vya kudumu na hatimaye, watatumbukia kwenye umaskini wa hali na kipato!

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, iwe ni fursa kwa wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kutambua kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Kazi ambayo mtu ameichagua kwa hiyari yake mwenyewe inachangia kwa kiasi kikubwa mchakato wa maendeleo ya Jamii inayomzunguka; kwa kukidhi mahitaji ya familia pamoja na kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya mtu binafsi, kifamilia na katika maisha ya kiroho.







All the contents on this site are copyrighted ©.