2014-05-01 09:06:57

Askofu Nyaisonga kusimikwa Jimboni Mpanda tarehe 4 Mei 2014


Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, waamini wa Jimbo la Mpanda wamesali kwa ajili ya kumwomba Roho Mtakatifu awajalie mchungaji mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda baada ya kifo cha Askofu Paschal Kikoti, kilichotokea kunako Mwaka 2012. RealAudioMP3

Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Mpanda, lilifurahi sana kusikia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Gervas Nyaisonga kutoka Jimbo Katoliki la Dodoma kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Tayari maandalizi ya mapokezi yamekamilika. Tarehe 2 Mei 2014, Askofu Gervas Nyaisonga na ujumbe wake kutoka Jimbo Katoliki la Dodoma watapokelewa Jimbo kuu la Tabora, tayari kuelekea Jimbo Katoliki la Mpanda.

Tarehe 3 Mei 2014, Askofu Nyaisonga atapokelewa rasmi Jimboni Mpanda na kukabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Mpanda. Jumapili tarehe 4 Mei 2014 atasimikwa rasmi kuwa ni Askofu wa pili Jimbo Katoliki Mpanda.

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda anasema, Askofu mkuu Ruzoka inamshukuru Mungu kwa wema na huruma yake kwa kuwapatia mchungaji mwingine kijana baada ya Jimbo la Mpanda kugubikwa kwa simanzi ya kifo cha Askofu Kikoti. Familia ya Mungu Jimboni Mpanda inaalikwa kuanza tena upya katika Kristo Yesu ili kujenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Askofu mkuu Ruzoka anasema, wamekutana mara kadhaa na Askofu Nyaisonga tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuliongoza Jimbo Katoliki la Mpanda. Anasema, Askofu Nyaisonga ni kijana na mchapakazi, bila shaka atasaidia mchakato wa Uinjilishaji Jimbo Katoliki la Mpanda na Ukanda wote wa Jimbo kuu la Tabora.







All the contents on this site are copyrighted ©.