Wanawake waandamana Nigeria kupinga vitendo vya Boko Haram
Wanawake na wadau mbali mbali nchini Nigeria, Jumatano tarehe 30 Aprili 2014 wameamua
kujitokeza hadharani kupinga vitendo vya mauaji, utekaji nyara na udhalilishaji wa
utu na heshima ya binadamu vinavyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini
Nigeria.
Wanawake hawa wanataka Kikundi cha Boko Haram kuwaachilia mara moja
wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara hivi karibuni. Maandamano makubwa yameandaliwa
na wanawake kutoka Jimbo la Borno, ngome ya Kikundi cha Boko Haram na kuungwa mkono
na vyombo vya habari nchini Nigeria.
Wanawake nchini Nigeria wameamua kuweka
kando tofauti zao za kiimani, kiitikadi na kikabila ili kuonesha mshikamano wa dhati
unaopania kuweka shinikizo zaidi kwa Boko Haram ili kuweze kuwaachia wasichana waliotekwa
nyara na wengi wao bado hawajapatikana na wala hawajulikani waliko hadi sasa. Wazazi
wanasema bado kuna wasichana 234 ambao wako mikononi mwa Kikundi cha Boko Haram tangu
walipotekwa nyara.