2014-04-30 09:13:57

Miaka 40 ya uhusiano kati ya Australia na Vatican, lengo ni kutetea mafao ya wengi!


Vatican na Australia zinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka arobaini ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Historia ya Australia imejikita katika huduma makini inayotolewa na Kanisa katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Australia, lakini zaidi katika sekta ya elimu, huduma msingi za afya na matendo ya huruma.

Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Australia wamejitahidi kuwa kweli ni wafanyakazi wema na waaminifu katika kuwahudumia jirani zao kwa hali na mali. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu jioni, tarehe 28 Aprili 2014 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka arobaini ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Australia na miaka mia moja tangu Vatican ilipoanza kutuma mwakilishi wake nchini Australia. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka mjini Vatican na Australia.

Katika mahubiri yake, Kardinali Pietro Parolin amewataka waamini kutoka Australia kumwangalia na kuiga maisha ya Mtakatifu Maria wa Msalaba MacKillop aliyeishi kunako mwaka 1842 hadi mwaka 1909; mwanzilishi wa Shirika la Mtakatifu Yosefu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri kunako tarehe 19 Januari 1995 Jimbo kuu la Sydney, wakati wa hija ya kichungaji ya Papa Yohane Paulo II Oceania.

Tarehe 17 Oktoba 2010 akatangazwa na kuandikwa kwenye orodha ya watakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Kardinali Parolin anasema kwamba, bado kuna mambo mengi ambayo nchi hizi mbili zinapaswa kuyatekeleza licha ya ushirikiano unaojikita katika mapokeo, ili kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo, ili kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki msingi, mafao ya wengi na ushuhuda wa udugu na upendo kama anavyoendelea kuhimiza Baba Mtakatifu Francisko.

Hii ni changamoto na mwaliko wa kuiona sura na mfano wa Mungu kwa kila mwanadamu, ili kuheshimu utakatifu wa maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na kuwashirikisha wengine ile furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita, mengi yamefanywa na pande hizi mbili, kumbe, zinaweza kusonga mbele kwa imani na matumaini hata kwa siku za usoni, kwa kuwa waaminifu kwa Injili sanjari na kukazia umoja na mshikamano; amani na ukweli.

Kardinali Pietro Parolin anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, kuna haja kwa Australia na Vatican kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi; haki na amani; utu na heshima ya binadamu kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho kati ya watu. Hii ni dhamana nyeti inayohitaji subira na uvumilivu kwa ajili ya mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.