2014-04-30 08:16:35

Kazi inayoheshimu utu wa binadamu ni nyenzo msingi katika mapambano dhidi ya umaskini duniani!


Fursa za ajira na kazi inayoheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu ni nyenzo msingi katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani unaongezeka maradufu licha ya maboresho katika maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baraza la Kipapa la haki na amani katika semina ya siku mbili iliyofunguliwa siku ya Jumanne, tarehe 29 Aprili 2014. Semina hii inahudhuriwa na wajumbe kutoka Shirika la Kazi Duniani, ILO, Mashirika ya Kanisa Katoliki yanayojihusisha na masuala ya kazi pamoja na wadau wengine muhimu waliotia sahihi katika Waraka unaokazia umuhimu wa kuwa na kazi inayoheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu kwa ajili ya maendeleo endelevu mara baada ya mwaka 2015. Dhana hii imejadiliwa kwa kina na mapana katika siku yake ya kwanza.

Semina hii ya kimataifa inayofanyika mjini Roma imefunguliwa rasmi na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, kwa kuwashukuru watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II waliosimama kidete kulinda na kutetea masilahi ya wafanyakazi, haki na amani; mambo yanayojionesha kwa namna ya pekee katika kukazia fursa za ajira na kazi ambayo kimsingi ni kielelezo cha ukamilifu, utu na heshima ya binadamu kama sehemu ya mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani.

Kardinali Turkson anasema kwa uchungu kwamba, licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa uzalishaji viwandani sanjari na utandawazi, lakini umaskini unaendelea kunyanyasa mamillioni ya watu, kwa kusema katika lugha nyepesi, lakini ukweli ni kwamba, kuna mabillioni ya watu ambao wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa na binadamu katika karne ya ishirini na moja.

Tafiti mbali mbali zinaonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira, wengine wanafanya kazi katika mazingira na duni na kwa kiwango cha chini kabisa; mambo ambayo kimsingi yanachangia kuporomoka kwa heshima na thamani ya kazi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Pale ambako kuna maboresho makubwa ya fursa za ajira, hapo kuna cheche za maendeleo kwa wafanyakazi na familia zao; maboresho ya huduma ya elimu na afya; kimsingi hii ni fursa kubwa katika maendeleo ya jamii husika.

Wajumbe wa semina hii ya kimataifa wanachambua tema ya kazi si tu kama njia ya kupambana na baa la umaskini duniani, bali pia wanaangalia fursa za kazi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, wafanyakazi wahamiaji pamoja na mkakati wa utunzaji bora wa mazingira. Kuna haja anasema Kardinali Turkson kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta hali bora na zenye usalama zaidi, ili kukoleza jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo hadi sasa yamesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Wajumbe wa semina wanaongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na mchango wa Mapapa mbali mbali katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; maendeleo ya watu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; ukweli katika upendo. Yote haya anasema Kardinali Turkson yanaonesha kwamba, kazi na maendeleo ya mwanadamu ni sawa na chanda na pete, kamwe hayawezi kutenganishwa, kwani yanalenga mafao ya wengi. Bila kazi, mafao ya wengi yako mashakani.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji, Injili ya Furaha anafanya rejea katika dhana hii, kwa kukazia umuhimu wa elimu makini, huduma bora za afya na kazi inayojikita katika: uhuru, ubunifu, ushirikishwaji na mshikamano kama kielelezo makini cha utu na heshima ya binadamu, ulinzi na utetezi wa maisha.

Baba Mtakatifu anaendelea kuichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kutetea utu na heshima ya wafanyakazi. Ukosefu wa fursa za ajira ni jambo ambalo linahatarisha na kugumisha hali ya watu wengi duniani. Kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa, inaonekana kwamba, ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingi umedumaa, hauna tena uwezo wa kujiongeza na kutengeneza fursa za ajira, kutokana na sababu msingi kwamba, fedha imepewa kipaumbele cha kwanza, utu na heshima ya binadamu vikawekwa rehani.

Kardinali Peter Turkson anaendelea kuwahimiza wachumi, watunga sera na wadau mbali mbali kujikita katika mchakato wa maendeleo ya uchumi yanayosimikwa katika misingi ya haki na mshikamano wa kidugu. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinapaswa kushughulikiwa kwa kina na mapana kwa kutumia nyenzo za ubunifu, ili kujenga na kuimarisha mifumo mipya ya ushirikiano wa kimataifa.

Semina hii ya kimataifa inahitimishwa Jumatano tarehe 3o Aprili, 2014 katika mkesha wa Siku kuu ya Wafanyakazi, yaani Mei Mosi, ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa, huku watu wengi wakiwa bado wameelemewa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Wajumbe wamekazia kwamba, kazi ni nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.