2014-04-30 09:50:47

Hakuna usawa katika ndoa za watu wa jinsia moja!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawataka Wabunge wa nchi hiyo kuwa makini pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za ndoa na familia zinazoundwa kati ya bwana na bibi wanapojadili hoja binafsi iliyotolewa na mbunge mmoja anayetaka haki sawa kwa watu wanaofunga ndoa za jinsia moja bila kubaguliwa!

Kanisa linaamini na kufundisha kwamba, kila mtu ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa bila kubaguliwa. Kwa kuzingatia kweli na misingi ya Injili, Kanisa linapinga ubaguzi, nyanyaso na dhuluma na linataka kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kimsingi familia ya kweli inaundwa katika ushirikiano kati ya bwana na bibi kama sehemu ya mchakato wa kukamilishana kwa ajili ya kupata watoto na kuwalea kadiri ya mpango wa Mungu. Hizi ni tunu msingi zinazopaswa kusimamiwa na kuendelezwa na Serikali.

Ikumbukwe kwamba, watoto wana haki ya kuzaliwa na kulelewa katika mazingira bora ya familia inayoundwa na Baba na Mama, kama ambavyo anakazia Baba Mtakatifu Francisko. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba, inawaundia watoto mazingira bora ya maisha, ili kuweza kufikia ukomavu. Watoto wanapaswa kuishi na kulelewa katika mazingira ya familia ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo!

Dhana ya usawa katika masuala ya ndoa na familia inatumiwa vibaya na baadhi ya watu ndani ya Jamii, kwani bwana na bibi katika maisha ya ndoa wanakamilishana kadiri ya mpango wa Mungu. Ndoa ya watu wa jinsia moja si sehemu ya haki msingi za binadamu na hivyo haiwezi kuwa na haki sawa katika malezi na makuzi ya watoto.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawachangamotisha wabunge kusimama kidete kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazoundwa katika upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi, ili kupata watoto na kuwalea. Hakuna usawa wowote kati ya ndoa ya watu wa jinsia moja na ndoa inayoundwa na Bwana na Bibi.

Kanisa Katoliki pamoja na wadau wengine wanatambua na kuthamini taasisi ya ndoa kama chemchemi ya furaha na maisha; taasisi inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.