Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha,
kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 29 Aprili 2014 amezungumzia juu ya Jumuiya
ya kwanza ya waamini waliokuwa na roho moja na moyo mmoja katika mambo yote, hali
iliyowawezesha kujenga amani na utulivu sanjari na kuendelea kutoa ushuhuda kwa Kristo
mfufuka pamoja na kuwahudumia maskini na wahitaji.
Hawa ni watu waliozaliwa
kwa maji na Roho na Roho Mtakatifu, wakawa ni mwili mmoja na roho moja; wakajenga
amani, utulivu na msamaha kati yao. Hizi ndizo tunu msingi zinazopaswa kudumishwa
na Jumuiya ya waamini, bila kuvurugwa na wivu usiokuwa na mashiko wala maendeleo kwa
Watu wa Mungu; mambo yanyosababishwa na Shetani. Jumuiya bado inaendelea kujengwa
na matatizo yatakuwepo, kwani haya ni mapambano yanayojikita katika mafundisho na
Mapokeo pamoja na kuwania madaraka.
Jumuiya ya kwanza ya Wakristo ilisimikwa
na kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, ikajipambanua kwa mshikamano wa udugu na upendo;
ikawa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya
za Kikristo kujipima kwa wakati huu, ikiwa kama: Jumuiya, Parokia au Majimbo haya
yanatoa ushuhuda wa kweli wa Yesu Kristo mfufuka, anayeendelea kuwa kati ya watu wake.
Jumuiya
za Kikristo hazina budi kujielekeza kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ni ushuhuda amini wa uwepo wa Roho Mtakatifu
anayetenda kazi ndani ya Kanisa, pamoja na kulichangamotisha kujenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa dhati.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaomba waamini kumwomba
Roho Mtakatifu awasaidie kutembea katika njia hii kwa kuonesha ile nguvu waliyoipata
kutokana na Ubatizo katika maji na Roho Mtakatifu.