2014-04-29 09:10:16

SADC yaombwa na IMBISA kusimama kidete kudhibiti vita na vurugu Kusini mwa Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kusini mwa Afrika, IMBISA limeiandikia Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika ujumbe mahususi kwa kuitaka kusimama kidete katika kudhibiti vurugu, ghasia na chokochoko za kijamii zinazoendelea kufuka moshi, Kusini mwa Afrika, kwani ni kheri kuzuia kuliko kuponya! IMBISA inasikitishwa kuona kwamba, vurugu na vita inaendelea kushamiri siku hadi siku huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Nigeria na Sudan.

IMBISA inasema, kuna makundi makubwa ya watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, umaskini, baa la njaa na kinzani za kijamii, hali ambayo inatishia amani, usalama na utulivu Kusini mwa Afrika. Kuna watu wanatafuta hifadhi Nchini Afrika ya Kusini lakini wanakumbana na vizingiti katika kufikia lengo lao, jambo ambalo linahitaji suluhu ya: kitaifa, kikanda na kimataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utawala bora unaozingatia sheria za nchi na zile za kimataifa. Watu hawana budi kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu.

IMBISA inaiomba SADC kusaidia mchakato wa kusitisha kinzani na vita inayoendelea chini kwa chini nchini Msumbiji, kwa kuimarisha majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, heshima na mafao ya wengi bila ya kukimbilia katika matumizi ya mtutu wa bunduki ambao umasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni mwaliko kwa SADC kusaidia nchi wanachama kuibua mbinu mkakati wa kukuza na kuimarisha uchumi kwa kuendelea kutumia rasilimali watu na vitu vilivyoko katika nchi hizi.

Tatizo la wakimbizi na wahamiaji linaweza kupunguzwa makali kwa kuwawezesha wakimbizi na wahamiaji kushiriki katika ujenzi wa uchumi pamoja na kuboresha maisha ya watu hawa. Kanisa linaendelea kushiriki katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu Kusini mwa Afrika kwani hakuna mgeni ndani ya Kanisa na wala ubaguzi wa rangi hauna tena nafasi katika maisha na maendeleo ya watu Kusini mwa Afrika.

Kinzani za kikabila ni mchezo mchafu uliopitwa na wakati, kwani kwa sasa watu wanandoto ya kutaka kuona umoja na mshikamano miongoni mwa Nchi za Kiafrika. Ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji ni dhamana ya kimaadili na kwamba, Kanisa litaendelea kutoa huduma kwa wahamiaji na wakimbizi, lakini viongozi wa Bara la Afrika hawana budi kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji kwa kujikita katika utawala wa sheria, mafao ya wengi pamoja na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Majadiliano yaendelee kupewa kipaumbele cha pekee katika kuzuia na kupata suluhu ya kinzani na migogoro mbali mbali Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.