Papa Francisko anawaalika vijana kutoka kimasomaso kukutana na Yesu Mfufuka!
Vijana wanaalikwa kumwangalia kwa namna ya pekee kabisa yule kijana tajiri anayesimuliwa
kwenye Maandiko Matakatifu aliyemwendea Yesu akiomba ushauri ili aweze kuurithi uzima
wa milele. Mitume wengi walikuwa ni vijana na walifurahia sana walipokutana na kuzungumza
na Yesu, kiasi hata cha kuwabadilishia mwelekeo wa maisha, kwani waliweza kusikiliza
ufafanuzi wa Neno la Mungu kwa kina na mapana!
Baba Mtakatifu Francisko katika
ujumbe wake wa video kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Kikanda nchini Argentina,
iliyoadhimishwa, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2014 nchini Argentina, katika mkesha wa
kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, anawauliza
vijana, jinsi walivyojisikia kwa mara ya kwanza walipokutana na Yesu katika hija ya
maisha yao ya kiroho, Anawaalika kuwaangalia Mitume waliokutana na Yesu kwa mara ya
kwanza katika maisha yao.
Yesu alionesha upendo wa pekee kwa yule kijana tajiri
aliyejitahidi katika maisha yake kushika Amri za Mungu, lakini akakosa ndani mwake
ufukara wa maisha ya kiroho, ndiyo maana anapoambiwa kwenda kuuza vyote alivyonavyo
na kuwapatia maskini, kisha amfuate Yesu, anashikwa na huzuni kubwa katika moyo wake.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, Maandiko Mataktifu yamesheheni mifano ya vijana wa kila
aina. Anawakumbusha yule kijana aliyeomba urithi kutoka kwa Baba mwenye huruma, kisha
akatokomea mjini kwenda kuponda mali na baadaye akakiona cha mtema kuni kwa kukumbana
uso kwa uso na baa la njaa! Hapa akajifunza kutubu na kuongoka, ili kukimbilia tena
huruma ya Mungu. Daima Baba yake alikuwa anamsubiri kwa hamu kubwa, kuona kijana wake
akirudi tena nyumbani. Siku ile aliporejea nyumbani, akamkumbatia na kumwonjesha tena
huruma na upendo usiokuwa na kifani.
Baba Mtakatifu amewakumbusha vijana wa
Argentina kuhusu yule kijana wa Naini aliyekuwa amefariki dunia baadaye akafufuliwa
na Yesu, kwa kumwonea yule mama mjane huruma? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wao
wanajisikia kuwa sehemu gani kati ya vijana wanaosimuliwa kwenye Injili? Je, wanaonesha
ari na shauku ya kuwashirikisha wengine ushuhuda wa kukutana na Yesu? Au wamekata
tamaa na kujikunyata? Au pengine tayari wamekwisha kupoteza maisha ya kiroho ndani
mwao?
Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha vijana kuendelea kuwa waaminifu
kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo, ili kujenga
na kuimarisha amani na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake sanjari
na kukumbatia Injili ya maisha pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wengine kama alivyofanya
Bikira Maria kwenye arusi ya Kana na mwishoni akasimama chini ya Msalaba wa Kristo.
Baba
Mtakatifu Francisko anawataka wasichana kuiga mfano wa Bikira Maria na wanawake watakatifu
wanaosimuliwa katika Injili kwa kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa
lake, wakimwachia Yesu nafasi ya kuwaongoza, ili waweze kukua na kukomaa, tayari kuwahudimia
Watu wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu amewatakia
kheri na baraka vijana hao katika maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Argentina Kikanda,
ili wapate nafasi ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, bila kuwa na woga
wala makunyanzi, bali wawangalie Yesu na Bikira Maria, ili waweze kusonga mbele, tayari
kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.