2014-04-29 07:22:14

Mbinu mkakati wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani


Jumuiya ya kimataifa na wadau mbali mbali hawana budi kujifunga kibwebwe ili kuheshimu, kulinda, kuhamasisha na kutekeleza dhamana ya haki ya chakula kwa wote, ili kupunguza idadi ya watu wanaokufa na baa la njaa duniani wakati kuna chakula kingi kinazalishwa lakini kinatupwa kama taka! Watu wana haki ya kupata lishe bora, kuishi katika mazingira bora kadiri ya mazingira yao. RealAudioMP3

Ni kweli kwamba, Jumuiya ya Kimataifa imefanya maendeleo makubwa katika mchakato wa upatikanaji wa chakula duniani tangu mara baada ya Vita kuu ya pili wa dunia, lakini baa la njaa bado lina waandama watu wengi zaidi duniani, kwani takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu million 840 wanaoteseka na baa la njaa duniani, wengi wao ni wale wanaotoka katika Nchi zinazoendelea duniani.

Watu hawa wanakabiliwa na kifo kinachoendelea kukwapua maisha ya watu pole pole kutokana na utapiamlo wa kutisha, hali ambayo inawanyima watoto fursa ya kukua na kukomaa pamoja na kujipatia maendeleo katika sekta mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao makuu mjini Geneva , wakati alipokuwa anachangia kwenye mkutano wa Baraza la haki msingi za binadamu la Umoja wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, utapiamlo wa kutisha na baa la njaa kamwe yasigeuzwe kuwa ni mambo ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweka mikakati madhubuti kisheria, itakayowezesha kuunda sera makini za haki ya chakula, udhibiti na ugavi wa rasilimali katika mapambano ya baa la njaa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuzingatia madhara yanayotokana na baa la njaa kama yanayopembuliwa na takwimu mbali mbali zinazooneshwa na Jumuiya ya Kimataifa; uzalishaji na ugavi wa chakula pamoja na kuzijengea Familia uwezo wa kununua chakula kwa bei nafuu. Ili kuweza kupata mafanikio katika mikakati hii kuna haja ya kubadili mfumo wa maisha, kuondokana na ubinafsi, kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine, kwa kuwa na uchu wa kupata faida kubwa.

Haki ya chakula inaweza kupatikana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajenga na kudumisha mshikamano wa kidugu pamoja na kuwajengea uwezo wakulima wadogo wadogo ili waweze kuongeza tija na uzalishaji katika mazao ya biashara na chakula. Wanawake katika nchi zinazoendelea ni wadau wakuu wa shughuli za kilimo na uzalishaji, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwawezesha wanawake kutekeleza dhamana hii kikamilifu zaidi. Msaada kwa wakulima hauna budi kuwashirikisha wadau wote kwa kuwalinda na kuwapatia haki ya kuzalisha na soko la uhakika wa mazao yao bila ya ubaguzi ambao mara nyingi unafanywa na Mataifa makubwa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema mshikamano wa kimataifa ni nyenzo msingi katika mapambano ya kuwa na haki ya chakula duniani pamoja na kukabiliana na majanga ya maisha yanayoibuka kila kukicha. Maadhimisho ya Mwaka wa Familia ya Wakulima Kimataifa iwe ni fursa ya kuhakikisha kwamba, haki ya chakula inapatikana kwa wote, kwa njia ya majiundo makini ya mshikamano kimataifa. Ni changamoto ya kuondokana na utamaduni wa utandawazi usioguswa wala kujali mahangaiko ya watu wengine, bali utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.