Kila mwananchi ana dhamana kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho
wa kweli!
Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma ambaye hivi karibuni aliteuliwa na
Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda, Tanzania katika
mahojiano na Radio Vatican anakazia umuhimu wa Mama Kanisa, Serikali na Jamii kwa
ujumla wake, kukazia umuhimu wa haki, amani na upatanisho wa kweli, kwani utapanisho
na haki ni msingi ya amani ya kweli!
Amani ya kweli
inajikita katika haki, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, upatanisho ni jambo
linalotangulia masuala ya kisiasa, kwani hii ni nguvu inayopata chimbuko lake kutoka
katika undani wa mtu. Ni jukumu la kila mwananchi kujikita katika kutafuta na kudumisha
misingi ya haki, amani na upatanisho pamoja na kujenga mifumo itakayoimarisha misingi
hii katika Jamii. Upendo wa kweli kati ya watu ni chemchemi ya amani.
Jamii
haina budi kujikita katika ujenzi wa utawala bora unaozingatia sheria na kanuni za
nchi. Ikiwa kama Serikali zinashindwa kudhibiti migogoro midogo midogo kuna hatari
kwamba, haki na amani inaweza kutoweka na hivyo kusababisha majanga katika jamii ya
watu. Kero na migongano kati ya wakulima na wafugaji ni mambo yanayopaswa kuangaliwa
kwa umakini mkubwa!
Kashfa za kidini na ushabiki wa kisiasa anasema Askofu
Nyaisonga ni mambo yanayoweza kusababisha kutoweka kwa misingi ya haki na amani. Kila
mwananchi ana wajibu wa dhamana ya kukuza na kuendeleza misingi ya haki, amani na
upatanisho.