Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, alikuwa ni kati
ya Watu wa Mungu waliohudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza Wenyeheri
Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni Watakatifu, Ibada iliyoongozwa na Baba Mtakatifu
Francisko, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili
ya huruma ya Mungu, tarehe 27 Aprili 2014.
Kardinali
Pengo katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakiri kwamba, bado kuna watu wana
imani kuhusu uwepo wa Mungu na utakatifu wa maisha ya viongozi wa Kanisa, kama ilivyojidhihirisha
kwenye kesha na hatimaye maadhimisho ya Siku kuu ya Imani kwa ajili ya kuwatangaza
Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni watakatifu.
Kardinali Pengo
anasema, licha ya afya yake kuwa si nzuri kwa siku za hivi karibuni lakini ameona
kwamba, ni jambo la muhimu kuweza kuhudhuria katika tukio hili la kihistoria ambalo
linamgusa kama mwamini binafsi na Kanisa la Tanzania na Kanisa la Kiulimwengu katika
ujumla wake. Mtakatifu Yohane XXIII anakumbukwa na watanzania kwa kuwaandikia Sala
ya kuombea Tanzania na kwa kuwapatia Kardinali wa kwanza Mwafrika. Ni kiongozi aliyethubutu
kwa ujasiri mkubwa kuitisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuleta
mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.
Mtakatifu Yohane XXIII alianza
utume wake wakati watu wamekata tamaa kutokana na mateso pamoja na mahangaiko ya Vita
kuu ya Pili ya Dunia, kiasi kwamba, watu wakapoteza imani. Kitendo cha kuitisha Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican, ni kielelezo cha utakatifu na ushujaa wa imani hasa kutokana
na mazingira na hali iliyokuwepo kwa wakati ule. Mtakatifu Yohane XXIII alilitaka
Kanisa kujikita katika mchakato wa kufanya upya, "aggiornamento", ili kurekebisha
mambo na kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa.
Kardinali
Pengo anasema kwamba, dhambi inawakatisha watu tamaa, lakini kwa njia ya imani thabiti,
watu wanaweza kupiga moyo konde na kuanza tena safari ya maisha yao, kwa kutambua
kwamba, daima kuna fursa ya kuweza kuanza upya na kufanya marekebisho makubwa katika
maisha, hizi ni cheche za utakatifu wa maisha. Kufanya mambo mapya ni mwaliko kwa
wa kupiga hatua ya kutenda mema zaidi. Mtakatifu Yohane XXIII anakumbukwa na wengi
kama "Baba Mtakatifu mwema", hali inayodhihirisha madai ya kubadilika ili kufikia
utakatifu wa maisha!