Mtakatifu Yohane XXIII: Uinjilishaji, Majadiliano na Amani!
Mtakatifu Angelo Giuseppe Roncali alizaliwa Bergamo, Kaskazini mwa Italia, tarehe
25 Novemba 1881 na kubatizwa siku hiyo hiyo. Alipata Kipaimara na Komunio ya kwanza
kunako mwaka 1889 na mwaka 1892 akaingia Seminarini. Alikuwa na kipaji cha uandishi
wa habari na makala zake zimekusanywa katika kitabu kinachojulikana kama "Giornale
dell'anima".
Kati ya mwaka
1901 hadi mwaka 1905 alipelekwa kusoma kwenye Seminari kuu ya Kipapa, Jimbo kuu la
Roma na baadaye, akaenda Jeshini kwa mujibu wa sheria. Tarehe 10 Agosti 1904 akapewa
daraja takatifu la Upadre.. Mwaka 1905 akachaguliwa kuwa Katibu wa Askofu Giacomo
Maria Radini Tedeschi hadi mwaka 1914. Akamsaidia Askofu wake katika kutekeleza utume
wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bergamo.
Aliwahi pia kufundisha pamoja na kufanya marekebisho katika Katiba ya Vijana Wakatoliki
Italia. Alikuwa anashiriki kuandika makala kwenye Gazeti la Jimbo Katoliki Bergamo
na kwamba, alikuwa ni mhubiri mahiri na makini.
Katika tafiti zake alibahatika
kukutana na watakatifu Charles Borromeo na Mtakatifu Francisko wa sale na kwamba,
hiki kilikuwa ni kipindi cha mwamko na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya
Kanisa. Askofu Radini Tedeschi akafariki dunia kunako mwaka 1914 na Padre Angelo Roncali
akaendelea na utumishi wake wa Kipadre na mwalimu Seminarini.
Wakati Italia
ilipotumbukia katika vita kunako mwaka 1914, aliitwa kuwa ni Padre wa maisha ya kiroho
kwa Askari waliokuwa mstari wa mbele. Baada ya vita alifungua nyumba kwa ajili ya
wanafunzi, ili kusaidia wanafunzi katika maisha yao ya kiroho. Kunako mwaka 1919 akateuliwa
kuwani Padre wa maisha ya kiroho. hapa akafunga ukurasa wa maisha yake, sehemu ya
kwanza.
Kunako Mwaka 1921 aliitwa mjini Vatican na Papa Benedikto wa kumi na
tano, kama Rais wa Italia katika Baraza kuu la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Kunako
mwaka 1925 Papa Pio XI akamteua kuwa Balozi wa Vatican nchini Bulgaria na hivyo kumpandisha
hadhi kuwa ni Askofu na kauli mbiu yake ilikuwa ni "Oboedientia et pax" "Utii na Amani",
mambo aliyoyapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Askofu na
baadaye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Akawekwa wakfu kama Askofu hapo tarehe 19
Machi 1925. Akatembelea na kuimarisha Jumuiya za Kikristo nchini Bulgaria,
Tarehe
27 Novemba 1935 aliteuliwa kuwa ni Mwakilishi wa Vatican nchini Uturuki, akajitosa
kimasomaso kwa ajili ya huduma ya Kanisa miongoni mwa vijana; akajenga na kuimarisha
majadiliano ya kidini. Wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia alijitahidi kuwasaidia
watu wengi waliokuwa wanateseka. Tarehe 20 Desemba 1944 Papa Pio XII akamteuwa kuwa
Balozi wa Vatican nchini Ufaransa. Wakati wa vita aliwasaidia sana wafungwa wa kisiasa,
akatekeleza utume wake katika hali ya unyenyekevu na akaendelea kuonesha utume wake
kama Padre. Alikuwa kweli ni mtu wa sala na tafakari ya kina.
Tarehe 12 Januari
1953 akateuliwa kuwa Kardinali na tarehe 25 Januari akateuliwa kuwa Patriaki wa Venezia,
akajitosa tena katika maisha ya kitume na shughuli za kichungaji, akaonesha ushupavu
na utakatifu wa maisha katika kazi za kichungaji, huku akijitahidi kufuata mifano
ya watangulizi wake hapo Venezia.
Baada ya kufariki dunia kwa Papa Pio XII
akachaguliwa tarehe 28 Oktoba 1958 kuwa Papa na akaamua kutumia jina la Yohane XXIII,
akajionesha ulimwenguni kama Mchungaji mwema; mnyenyekevu na mpole wa moyo, jasiri
na mwenye huruma, aliyemwilisha matendo ya huruma katika utume wake, kwa kuwatembelea
wagonjwa na wafungwa. Akakazia umuhimu wa Kanisa kuwa kweli ni Mwalimu na Mama kwa
kuandika Waraka wa kichungaji, "Mater et Magistra" wa Mwaka 1961 na "Pacem in Terris"
Amani Duniani mwa Mwaka 1963.
Aliitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma, akaunda
Tume ya kurekebisha Sheria za Kanisa na hatimaye, akaitisha maadhimisho ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican. Akatembelea Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, ili
kuwaimarisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni kiongozi aliyejikita katika
mchakato wa Uinjilishaji, majadiliano ya kiekumene pamoja na majadiliano na watu wote.
Tarehe 3 Juni 1963 akafariki dunia kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, akasindikizwa
na litania ya sala kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu Yohane
Paulo II tarehe 3 Septemba 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka Elfu
mbili ya Ukristo akamtangaza kuwa Mwenyeheri. Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 ametangazwa
kuwa Mtakatifu, matendo makuu ya Mungu.
Imehaririwa na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.