2014-04-27 10:40:54

Mtakatifu Yohane II: Umissionari, majadiliano, utu na heshima ya mwanadamu!


Karol Jozef Wojtyla alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki hapo tarehe 16 Oktoba 1978. Alizaliwa kunako tarehe 18 Mei 1920 mjini Wadowice, Poland. Akiwa na umri wa miaka tisa akapokea Komunio ya kwanza na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara akiwa na umri wa miaka kumi na tisa. Kati ya Mwaka 1940 hadi mwaka 1944 alifanya kazi kwenye kiwanda cha Kemikali cha Solvay, ili kujipatia mahitaji yake msingi na kukwepa kupelekwa uhamishoni nchini Ujerumani. RealAudioMP3

Kuanzia Mwaka 1942 alishiriki katika majiundo ya Kipadre ufichoni yaliyokuwa yanatolewa na Askofu mkuu Adam Stefan Sapieha na wakati huo huo alikuwa anashiriki pia katika michezo ya kuigiza. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia akaendelea na masomo yake ya falsafa na taalimungu na hatimaye akapadrishwa hapo tarehe Mosi, Novemba 1946.

Baadaye akatumwa kwenda Roma kuendelea na masomo ya juu ambako alijipatia shahada ya uzamili katika taalimungu kunako mwaka 1948, tema aliyochagua ilikuwa ni imani mintarafu kazi za Mtakatifu Yohane wa Msalaba. Wakati wa masomo yake mjini Roma, aliendelea kutoa huduma za kichungaji kwa wahamiaji na wageni kutoka Poland waliokuwa wanaishi Ufaransa, Ubelgiji na Ireland. Alipohitimu masomo yake na kurudi Poland alipangia kazi: Parokiani, akawa ni mlezi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu na baadaye akaendelea na masomo yake. Akawa Jaalimu wa falsafa na taalimungu kwenye Seminari kuu ya Krakovia na Lublino.

Tarehe 4 Julai 1958 akateuliwa na Papa Pio XII kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Krakovia. Akawekwa wakfu tarehe 28 Septemba 1958. Tarehe 13 Januari 1964 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Krakovia. Papa Paulo VI akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 26 Juni 1967. Alishikiri kikamilifu katika Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Tarehe 16 Oktoba 1978 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wakati wa utume na maisha yake, alibahatika kufanya hija za kichungaji nchini Italia 146, akatembelea parokia 317 kati ya Parokia 332 za Jimbo kuu la Roma. Amefanya hija za kichungaji 104 sehemu mbali mbali za dunia. Ameandika vitabu kadhaa. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alifanikiwa kuadhimisha Ibada 147 za kuwatangaza watumishi wa Mungu kuwa Wenyeheri ambao idadi yao ni 1338 na Watakatifu 482. Amewateua Makardinali 231. Tangu mwaka 1978 ameadhimisha Sinodi 15.

Tarehe 13 Mei 1981 alipigwa risasi, lakini kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu aliweza kupona na hatimaye, kuonana na mtu aliyempiga risasi, akazungumza naye na kumsamehe. Papa Yohane Paulo II akaendelea na utume wake kwa ari na ujasiri mkubwa. Akaanzisha Majimbo, ili kupeleka huduma za kichungaji karibu na waamini, akafanya marekebisho makubwa katika Sheria za Kanisa, akaruhusu kuandikwa kwa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na kuliwezesha Kanisa kuadhimisha matukio makubwa katika maisha na utume wake. Alibahatika kukutana na waamini, mahujaji na wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia mjini Vatican. Wakuu wa nchi na watu mashuhuri walipata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Papa Yohane Paulo II.

Papa Yohane Paulo II alifariki dunia tarehe 2 Aprili 2005, katika mkesha wa Jumapili ya Huruma ya Mungu, aliyokuwa ameianzisha. Akazikwa tarehe 8 Aprili 2005. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamtangaza kuwa Mwenyeheri hapo tarehe Mosi, Mei 2011. Tarehe 27 Aprili 2014, Kanisa linamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kumtangaza Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.