2014-04-26 15:05:51

Woga na mashaka ni sumu ya imani


Katika dominika hii ya pili ya Pasaka, Injili inatuletea aina mbili za mazingira yaliyo tofauti:Mazingira ya kwanza, Yesu anawatokea wafuasi jioni ya siku ileile ya Pasaka, wakiwa chumbani pindi mtume mmoja aitwaye Thomas hakuwepo. Mazingira ya pili, ni siku nane baadaye Yesu anawatokea tena wafuasi chumbani sasa akiwepo hata Thomas. Mazingira ya kutokea-tokea kwa Yesu baada ya ufufuko wake ni tofauti hasa ukikumbuka alivyomtokea mara ya kwanza Maria Magdalena asubuhi ileile ya Pasaka.

Mazingira aliyomtokea nayo yalikuwa ni ya nje kwenye bustani karibu na kaburi. Lakini kwa mitume ilikuwa ni jioni tena chumbani milango ikiwa imefungwa kutokana na woga wa wanafunzi. Mwinjili anataka kutuonesha kwamba Yesu anafika katika ulimwengu kwa namna ambayo si ya kiyakinifu, ni yeye lakini siyo yuleyule. Kitu cha muhimu zaidi kukiepa hapa ni matumizi ya neno hili “kutokea”, kwa sababu neno hili halijatumika kabisa na mwinjili. Fasuli inasema, Yesu alikuja na kusimama katikati. “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwa wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi: akaja Yesu akasimama katikati, akawaambia, “Amani iwe kwenu.” (Yoh. 20:19).

Siku ya Pasaka na siku nane baadaye Bwana anakuja na kukaa katika jumuia yake iliyokusanyika pamoja, na kama ilivyokuwa kwa wafuasi wale wa mwanzo siku ya Pasaka kadhalika waumini siku ya Pasaka. Waumini hao hawana budi kufungua sana macho yao, lakini siyo macho ya kiyakinifu, yanayoangalia kwa udadisi na kuanisha mambo, bali kwa macho safi, macho ya imani yanayoweza kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida.

Ndivyo inavyotufundisha Injili ya leo jinsi ya kufungua macho ya imani na kuangalia Yesu mfufuka anayefika na kukaa kati ya jumuia iliyokusanyika pamoja. Wafuasi wanashangaa kwa kutokewa na Bwana kwani walikuwa na woga sana. Wamekusanyika pamoja siyo kutokana na upendo waliokuwa nao kati yao, la hasha, bali kutokana na woga, kwa vile wanaye adui mmoja wanayemwogopa yaani wayahudi.

Angalia watu wengine wanaotembea nje, wanawaacha tu hawa wafuasi wajifungie humo chumbani, wao hawana wasiwasi wowote kwani ni kesi binafsi ya mitume walioingiwa na wasiwasi kutokana na yaliyotokea. Hawa wanao woga kwa vile hawajamwona Bwana mfufuka na kuhuishwa na roho ya mfufuka, hivi wanao woga. Woga huo unawapata pia wakristu wowote katika jumuia kama endapo wanakuwa hawana mang’amuzi ya Kristu mfufuka. Hali hiyohiyo inaweza kumkumba kila mkristu mkereketwa na Kristu kama anakosa mang’amuzi ya Kristu mfufuka katikati ya ndugu zake.

Woga huo wa Mkristu unatokana na mambo mawili: Mosi, kuogopa kifo. Mkristu aliyemwona Kristu anayeingia katika utukufu wa Baba hawezi kuwa na woga wowote ule wa kifo. Anaweza kuwa na woga wa homa, ugonjwa, mateso, lakini siyo wa kifo. Mtu huyo atasubiri kama “mlinzi akeshavyo akisubiri kuchomoza kwa jua la asubuhi”.

Kuingia kwake makaoni kwa Baba yake ambako ni lengo la wote, hakuwezi kumpatia woga wa kifo. Hata kama woga huo unabaki kutokana na kuachana na wapenzi wake na vitu mbalimbali ambavyo Mungu ametupatia. Kwa hiyo hapa unauona woga wa wanafunzi, ambao walikuwa bado hawajamwona Kristu mfufuka.

Woga wa pili, unakuwa dhidi ya wengine ambao hawakuyapokea mapendekezo haya ya Yesu hadi wakataka kumfifisha kabisa. Wenye woga aina hiyo hawawezi kuwa wanafunzi wa kweli, kwani Yesu anawatuma wafuasi wake kama vile kondoo kati ya mbwa mwitu. Kama unao woga kwa mbwa mwitu, basi ni bora kutoroka na kwenda mbali kujificha.

Kadhalika woga ni ni kitu kibaya kupita kila kitu kingine katika imani, kwa sababu unawafanya wafuasi wa dini kuwa wenye msimamo mkali, hawaambiliki, hawataki majadiliano, ni wagomvi, ni wachokozi, wanapiga makelele, wanapenda zogo katika kuitangaza imani yao.

Kwa sababu kama imani yao na wanachokisadiki kingekuwa cha ukweli na wanakiamini kwa dhati, basi wasingekipigia makelele, badala yake wangekitangaza kwa furaha na kwa utulivu. Pengine ingekuwa pia njia ya kujisaidia wao wenyewe ya kuuona mwanga wa Pasaka. Kwa hiyo yatubidi tujiangalie sana, kwani woga unatuingiza katika hatari ya kujifungia katika ukweli wetu usio na msingi wa kuchochewa tu na mapokeo wa mambo yale tuliyozoea kuyatenda, tunakuwa viziwi mbele ya hali halisi na hivi kujikuta unajihami mbele ya kosoo ya imani yako, na unakuwa mwoga wa mambo mapya.

Katika kipindi fulani cha historia ya Wakristu, Kanisa lilikuwa na hofu kubwa sana wakati Biblia ilipokuwa inamilikiwa na Waprotestanti. Kulikuwa pia woga wa demokrasia, na ule woga wa kukutana na utamaduni au mila nyingine ngeni. Woga aina hiyo ni sawa na ule wa mitume wa kujifungia ndani ya chumba. Yaani unakuwa na woga na mambo ya nje.

Huku kujitenga na kujifungia ndani ya chumba katika nyumba moja, kuna maana pia ya kiteolojia: Yohane anataka kuonesha kwamba mbele ya ulimwengu, wanafunzi wanajisikia katika mazingira mageni, wanayo thamani ambayo si sawa na zile za ulimwengu. Yesu anasema, ninyi mpo katika ulimwengu lakini si wa ulimwengu huu. Ndiyo maana wanakuwa na woga.

Aidha, endapo mmoja anajitangazia kwamba amemwona Kristu mfufuka, anatangaza imani yake, hivi anaogopa kueleweka kuwa ni kichaa, yaani ni mtu anayeishi nje ya ulimwengu, kwa sababu watu wamefungwa na mtindo wa maisha ya ulimwengu huu hawaoni namna nyingine ya maisha. Kwa mfano Mtakatifu Paulo anapozungumza juu ya ufufuko, watu wanamcheka na kumwambia waziwazi kwamba “juu ya suala hilo tutakusikiliza tena wakati mwingine”.

Ni ngumu sana kushuhudia imani yako hadharani. Hata mapadre, usiku wa Pasaka, hatuwi hata na uso wa furaha wa kuona mwanga wa ufufuko. Kwamba Yesu yuko na alifika kusimama mbele ya wafuasi. Yaani mwanzo mpya wa kudumu wa uwepo wa Yesu. Amefufuka na kuonesha mikono yake na kuwa katikati yao. Anaonesha mikono iliyofanya kazi na ubavu wake, hiyo ndiyo kadi yake ya utambulisho. Mikono iliyotenda mema na kupigiliwa misumari na moyo wake uliochomwa mkuki ilipotokea damu kuonesha maisha na maji kuonesha Roho mtakatifu, maisha yaliyomwagwa duniani maisha ya Roho yaliyotolewa ulimwengu. Hii ndiyo ID ya Yesu.

Mazingira ya pili, aliyotokea Yesu ni ya siku nane baada ya ufufuko. Tomasi hakuwepo pale alipotokea Yesu mara ya kwanza. Huyu Tomasi anaitwa Didimo maana yake Pacha, “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomas, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. .. Basi, baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomas pamoja. Akaja Yesu na milango imefungwa akasimama katikati , akasema, “Amani iwe kwenu.”(Yoh. 20: 24, 26). Mwinjili anasisitiza sana jina hili Pacha (Didimo). Yaonekana kuwa huyu ndiye pacha wa kila mmoja wetu. Kwa sababu hata sisi tutapita safari hiyohiyo ya jinsi ya kumfuata Kristu mfufuka.

Katika Injili, Thomasi anajitokeza mara tatu: Mara ya kwanza ni pale Yesu anapotaka kwenda Yudea, alikokufa Larazo, Thomas anasema twende tukafe sote huko: “Basi Tomas, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, “Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” (Yoh. 11:16). Kwa hiyo ni kweli Tomasi anayo mang’amuzi ya kifo tu, bali mang’amuzi ya ufufuko hana kwa sababu hajayashuhudia. Amebakiwa na wazo lake lilelile, “Twendeni tukafe naye”. Nafasi nyingine ni kwenye karamu ya mwisho, pale Yesu anapowaambia wanafunzi kwamba kule ninakoenda ninyi mnafahamu njia. Tomasi anasema, sisi hatujui unakoenda, tutawezaje kuijua njia? “Nami niendako mwaijua njia.” Tomas akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia?” (Yoh. 14:4-5) Huyu ndiye ndugu yetu Tomas, pacha wetu (Kurwa), kwa sababu anataka kujua. Kuna wakristu wengi wanaopata taabu ya kuelewa mambo yote katika imani. Anaye pacha wa Tomasi atauliza, “utuoneshe njia.” Kwani baada ya kuuliza Yesu anaweza kujieleza: “Mimi ni njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” (Yoh. 14:6).

Hebu tuangalie ni katika vipengee vipi Tomas anaweza kuwa ni pacha wako.
Hoja ya mojawapo yaweza kuwa Tomas alikuwa haelewi ni kwa nini wenzake wamejifungia chumbani. Yeye ameondoka na kwenda kuzubaa sijui wapi kwa sababu hajisikii kuwa na woga wowote ule. Katika kipengee hiki, Tomas ni pacha au kurwa wa mtu yule ambaye hajisikii kuwa wa maana au bora zaidi kuliko wengine, yaani, haelewi ni kwa nini wengine wamejifungia ndani.

Ni dhahiri kwamba Tomas siyo pacha wa wale wanaojitenga na jumuia ya kikristu kwa sababu labda wanachekwa na kudharauliwa na wengine; wanaojisikia bora zaidi na kuwahukumu wengine wasio katika jumuia au hata wanaowahukumu wale walio katika jumuia kwamba ni waovu kuliko wengine, au kama wale wanaoacha dini yao na kuingia nyingine.

Tomas hahukumu, wala kudharau wengine bali yawezekana anajiona kama amedanganyika kidogo au amekwazika na jumuia ile. Yaani ni kama wakristu wale wanaoona ndani ya kanisa kuna makwazo au mambo ya aibu, hivi wanajisikia kukwazika na kuteseka mioyoni mwao. Hivi wanaona ni bora kujiweka kidogo pembeni.

Aina ya nyingine ya kuwa pacha wa Tomas ni pale wale ambao wamedanganyika na muundo wa kanisa, na uendeshaji wa mambo ya kanisa, kukosa mpango mzuri. Hakuna uinjilishaji wa kutosha, au kuna utawala wa kibabe, kuna kujionesha ukuu unaotegemea mali, na hivi wanaona afadhali kujiepusha kidogo. Waumini wasioamini kama mambo yanaweza kubadilika katika kanisa. Hawa ni pacha wa Tomas.

Anapofika Tomas wenzake wanamhabarisha: “Tumemwona Bwana.” Kwa tamko hili walikuwa wanataka kummweleza kwamba mambo yamebadilika, si kama alivyodhani au kama alivyoyaacha. Tomas anataka kuhakikisha yeye mwenyewe kama kweli mazingira aliyoyaacha yamebadilika.

Hapa sasa tunakutana na pacha mwingine, yaani wale wanaotaka kuhakikisha kwa kuona na kugusa. Pacha wa Tomas ni wale wasiomwona Yesu wa Nazareti lakini wameitwa kumwamini ili kumshuhudia kwa ndugu zao. Pacha ni wale wasioelewa. Yaani hao pia wameitwa ili kuelewa lakini wanayo namna mbili ya kuelewa. Kimwili, kuamini kwao ni kama kule Tomas, lakini ndani yao kuna haja na hamu ya kuamini ambayo wanataka kuihakikisha.

Aliye na mang’amuzi haya ya ndani, ajue kwamba Tomas ni pacha wake. Na kwamba tusiwe na woga wa kuungama mashaka yetu ambayo ni kama ya Tomas, kama tunaweza kugusa kama Tomas hatuwezi kuwa na mashaka. Lakini kugusa huko kwetu hakuwezekani.

Kwa hiyo ni vyema kabisa kuwa ndani yetu tunaye huyo pacha wetu Tomas wa kuona mashaka kwamba huyo aliyetoa maisha kwa kufa kwake kama mtumwa ameingia katika utukufu wa Baba. Kwa hiyo fundisho kuu tunalopata hapa kwa huyu pacha wetu ni hili: Yesu anapofika siku ya nane anaonesha majeraha yake na anamwita Tomas kuja kuhakikisha.

Huo ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuweka mikono yetu ubavuni pake. Kualikwa na Yesu Mfufuka kuweka mikono yako ubavuni mwake maana yake pale unapoweka mikono yako, shughuli zako zote, na hasa ukijiweka wewe mwenyewe, kujiaminisha na kujitoka kabisa maisha yako kwa upendo kama ya Yesu hapo umeingia katika ulimwengu wa Mungu na wa utukufu wa ufufuo.

Upacha mwingine na Tomas ulio mzuri sana, ni pale Yesu anapomwalika Tomas kuyatupa maisha yake kwenye mapendekezo ya mwalimu: “Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh. 20: 27), naye Tomas anapojibu: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yoh. 20:28). Hilo ni ungamo la imani katika Mungu wa kweli imani inayojidhihirisha katika ufufuko wa Kristu. Imani kwa Mungu anayetoa maisha yake kwa ajili ya upendo.

Tomas aliyekuwa na mashaka, ndiye wa kwanza kushuhudia imani iliyo safi ya wakristu wa kwanza. Ni yeye aliyeona uthibiti wa msulibiwa katika ufufuko. Haamini juu ya Mungu anayeadhibu, anayezawadia, anayewapenda wema tu, amemwamini katika Kristu aliyetoa maisha Mungu wa kweli ambaye hawezi kuwa mwingine isipokuwa yule aliyesulibiwa kwa ajili ya upendo.

Uhakika kwamba ameona na kugusa mikono na ubavu wa Mungu, uhakika ule anaweza kuwa nao tu kwa mtazamo wa imani. Mtazamo unaotakiwa kuufungua daima pamoja na jumuia. Sisi tunasikia sauti ya Bwana na katika mkate wa Ekaristi sisi tunagusa mapendekezo yake ya maisha ya kujifanya mkate kwa ajili ya kutupenda.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.