Waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akutana na Papa mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na
Waziri mkuu wa Ukraine Bwana Arseniy Yatsenyuk na baadaye alikuwa na mazungumzo na
Kardinali Pietro Parolin aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Dominique Mamberti,
Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Mazungumzo
ya viongozi hawa wawili yalijikita katika masuala ya uhusiano kati ya pande hizi mbili;
hali tete inayoendelea kujitokeza nchini Ukraine, kwa matumaini kwamba, wadau wote
watajitahidi kushirikiana ili kurejesha hali ya amani na utulivu mintarafu sheria
za kimataifa pamoja na kudumisha uhusiano mwema kati ya watu.
Kwa namna ya
pekee, viongozi hawa wawili wamegusia mchango wa Makanisa na Mashirika ya kidini nchini
Ukraine na kwamba, wanachangamotishwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika mchakato
wa ujenzi wa amani na utulivu. Viongozi hawa wameonesha uwezekano wa Jumuiya ya Kimataifa
kushiriki zaidi katika mchakato huu.