2014-04-25 11:46:54

Yohane XXIII ni mtoto wa mkulima aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa!


Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni Watakatifu, Jumapili ijayo tarehe 27 Aprili 2014, Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam na ujumbe wa matashi mema kwa waamini na wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Italia kwa Mwenyeheri Yohane XXIII kutangazwa kuwa Mtakatifu. Miaka hamsini imekwisha kuyoyoma, lakini bado watu wengi wanamkumbuka kwa tabasamu na upole wake kama Baba mwema!

Baba Mtakatifu anaialika Familia ya Mungu, Kaskazini mwa Italia kumwimbia Mwenyezi mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi kubwa ya utakatifu ambayo amelizawadia Kanisa; imani ambayo inabubujika kutoka katika uhalisia wa maisha ya kawaida, kutoka kwa wakulima na wafanyakazi; familia zilizoonja upendo na ukarimu wa Mungu, kiasi hata cha kuweza kushirikisha wengine katika hali ya kawaida kabisa.

Mama Kanisa anawachangamotisha Watoto wake kujikita katika Uinjilishaji Mpya pamoja na kuwasindikiza watu katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili watu waweze kupata Maji ya Uzima wa Milele. Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yamekuwa ni chanzo kikuu cha utakatifu wa Mwenyeheri Yohane XXIII na kwamba, ni furaha kubwa tukio hili linamhusisha pia Yohane Paulo II, kiongozi aliyeleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa kiraia wataweza kujenga na kudumisha udugu na mshikamano.

Haya ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko yaliyoandikwa kwenye Gazeti la "Eco de Bergamo", gazeti ambalo Papa Yohane XXIII alishiriki kwa kuandika makala kwenye gazeti hili.







All the contents on this site are copyrighted ©.