Watanzania hawaridhishwi na malumbano yasiyokuwa na mashiko Bungeni!
Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Cleopa David Msuya amempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha
mchakato wa Katiba Mpya na amemshauri kutokuvunjwa moyo na kile ambacho amekielezea
kama “mambo madogo madogo” yanayoendelea ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
Aidha,
Mzee Msuya amesema kuwa Rais Kikwete hatasahauliwa kwa kipindi chake cha uongozi kutokana
na upanuzi mkubwa wa shughuli za maendeleo. Mzee Msuya ameyasema hayo Aprili 23, 2014
wakati alipozungumza kuwashukuru na kuwaaga wananchi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa
Kilimanjaro kufuatia hatua yake ya kunga’atuka katika uongozi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) wilayani humo, shughuli ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete iliyofanyika ofisi za CCM Wilaya ya
Mwanga.
Katika hotuba yake ndefu, Mheshimiwa Msuya ambaye ameshikilia nyadhifa
nyingi za uongozi nchini ikiwamo ile ya kuwa Mbunge wa Mwanga kwa miaka 20 mfululizo
amemwambia Rais Kikwete: “Tunakupongeza kwa kuanzisha uandaaji wa Katiba mpya itakayoongoza
Taifa letu la Tanzania kwa miaka 100 na zaidi ijayo. Zoezi hili likikamilika kama
ulivyoliweka itatuwezesha kusonga mbele na maendeleo ya umma kwa kasi zaidi chini
ya utawala bora unaotabirika. Hii ni shughuli kubwa na muhimu sana kwa wananchi wetu,
na Mheshimiwa Rais wala usivunjwe moyo na mambo madogo madogo ambayo yanatokea Dodoma,”amesema
Mzee Msuya.
Mheshimiwa Msuya ambaye alishikilia ubunge kwa jumla ya miaka 39,
ikiwamo 20 ya Ubunge wa Mwanga na anajulikana kama “Baba wa Mwanga”amemwambia Rais
Kikwete: “Tunakupongeza kwa maamuzi makubwa na mazito ya msingi uliyoyafanya kuonyesha
njia ya maendeleo kwa Taifa letu la Tanzania ikijumuisha Mwanga”.
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiamuru Wizara ya Uchukuzi
na taasisi zake kuchukua hatua za mara moja kukomesha aibu ya viwanja vya ndege vya
Tanzania kutumika katika uchochoro wa kupitisha na kusafirisha madawa ya kulevya.
Aidha,
Rais Kikwete amesema ukweli kuwa madawa ya kulevya yanazidi kupita katika viwanja
vya ndege za Julius Nyerere International Airport (JNIA) na ule wa Kilimanjaro International
Airport (KIA) unazidi kuchafua heshima na jina la Tanzania.
Rais Kikwete alikuwa
anazungumza Alhamisi, Aprili 24, 2014, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi
wa Awamu ya Tatu ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam kwenye
eneo la Uwanja huo. Rais ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Uwanja huo muda
mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Hospitali ya Kisasa ya Kufundishia
na Kutoa Huduma katika eneo la Mlongazila, eneo la Kibamba, Dar Es Salaam. Shughuli
zote mbili ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano.
“Siridhishwi na hali
ya usalama katika viwanja hivi viwili na matukio ya kusikia madawa yametokea Tanzania
kupitia viwanja vyake na yamekamatwa huko Australia yanachafua sana jina la nchi yetu.
Badala ya kuchukua hatua kukomesha jambo hili tunakwenda mbele, tunakwenda nyuma…mbele,
nyuma. Hili haliwezi kuruhusiwa kuendelea. Ni jambo la kutia simanzi sana,” amesema
Rais Kikwete na kuendelea:
“Mmeyasema wenyewe…leo kiwanja hiki kinapitisha
abiria milioni 2.5 kwa mwaka, mkifikisha abiria milioni sita si mtakuwa soko huria
kabisa…..mara leo mwanamuziki huyu kakamatwa Afrika Kusini…mara kesho yule….limalizeni
hili haraka. Nataka tuongeze usalama sana katika viwanja hivi viwili…. vimekuwa kama
uchochoro.”
Rais Kikwete amemtaka Waziri wa Uchukuzi kumjulisha ni maofisa
gani wa Idara za Serikali wanahusika kupitisha madawa hayo kwenye viwanja hivyo: “Kama
kuna maofisa wa ushuru, ama maofisa wa uhamiaji, ama maofisa wa polisi ama maofisa
wa uwanja wa ndege ambao wanashiriki katika mchezo huu wa kupitisha madawa haya nipeni
orodha yao, nitawaondoa kazini. Tusifanye masihara na hili, linatuaibisha sote. Tusiwaonee
aibu watu katika jambo hili.”