Kanisa linasimikwa katika furaha inayoshuhudiwa na Jumuiya ya waamini!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, jioni tarehe 24 Aprili 2014 ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani
baada ya Mama Kanisa kumtangaza Mwenyeheri Padre Josè de Anchieta, Mtume mwaminifu
wa Brazil kuwa Mtakatifu.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia umuhimu
wa waamini kutolea ushuhuda wa furaha inayobubujika baada ya kukutana tena na Kristo
mfufuka anayewakarimia amani na maisha tele, tayari kufukuza giza la wasi wasi na
hofu ya Wayahudi. Waamini wanapokutana na Yesu, wanapaswa kufurahia na kuwa na kiasi
kwa kukutana na Yesu Kristo Mfufuka.
Ni rahisi kwa waamini wengi kujitumbukiza
katika imani tepetevu ili kuwa na uhakika wa maisha yajayo badala ya kujenga imani
na matumaini kwa Kristo Mfufuka aliyeshinda dhambi na mauti. Ni rahisi kwa waamini
kuzama katika ndoto badala ya kuonesha unyenyekevu kwa Kristo Mfufuka anayewaalika
na kuwatuma, badala yake, wanajikuta wanajitenga na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Baba
Mtakatifu anasema, Mitume wa Yesu waligubikwa mno na wasi wasi kiasi hata cha kushindwa
kufurahia uwepo wa Kristo. Hii ndiyo hali halisi hata kwa Wakristo wa nyakati hizi.
Baba
Mtakatifu anasema, Mitume waliendelea kufanya miujiza kwa nguvu ya Yesu Mfufuka, kiasi
cha kuwaponya watu ambao waligeuka na kuwa ni mashahidi wa furaha ya ufufuko wa Kristo,
matendo makuu ya Mungu. Mtume Petro aliyekuwa mwoga, anapata ujasiri wa kumshuhudia
Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kikolezo muhimu cha kukua
na kukomaa kwa Kanisa linaloendelea kutolea ushuhuda wa Ufufuko wa Kristo. Kanisa
linasimikwa katika furaha inayoshuhudiwa na Jumuiya ya Waamini katika Habari Njema
ya Wokovu.
Baba Mtakatifu anasema, waamini wanayo dhamana ya kuwashirikisha
jirani zao Injili ya Furaha, ili kugundua maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo
na Kanisa lake. Mtakatifu Josè de Anchieta, alibahatika kuwashirikisha wengine ile
furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yake.
Ni kijana
aliyetumwa akiwa na umri wa miaka kumi na tisa nchini Brazil, akabahatika kutekeleza
utume wake kwa Kristo na Kanisa lake, akawa ni mwanga angavu katika maisha na ushuhuda
wake pamoja na kumtegemea Bikira Maria. Alikuwa ni mhubiri mkuu wa amani iliyokuwa
inabubujika kutoka katika Neno la Mungu pamoja na kushuhudia kwamba, Yesu amfufuka
kweli kweli!