Jitahidini kuzikabili changamoto za maisha kwa njia ya ushuhuda makini, mafundisho
ya Kanisa na kweli za Kiinjili!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 25 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na
Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linaloundwa na Botswana, Swaziland
na Afrika ya Kusini, ambalo linaendelea na hija ya kitume inayofanyika walau kila
baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican.
Baba Mtakatifu anawashukuru Maaskofu
kwa kumshirikisha imani na utume wa kutangaza Injili ya Kristo Kusini mwa Afrika,
eneo ambalo linaendelea kukua na kukomaa zaidi katika imani, matunda ya kazi za kimissionari.
Katika kipindi cha miaka mia mbili, Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika limeendelea
kuwekeza katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Kazi ya
Uinjilishaji inaendelea kwa kasi na ari kuu.
Baba Mtakatifu anasema, licha
ya magumu na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa kutokana na
umbali, uhaba wa rasilimali fedha na watu pamoja na kukosekana kwa huduma za Kisakramenti
kutokana na uhaba wa Mapadre, lakini Kanisa bado linaendelea kucharuka. Juhudi zinaendelea
kufanyika kwa ajili ya kuwatayarisha Mashemasi wa kudumu, ili kusaidia sehemu ambako
kuna uhaba wa Mapadre, juhudi ambazo zinapaswa kuimarishwa na majiundo makini kwa
Makatekista wanaoshiriki kutoa Katekesi kwa vijana wa kizazi kipya.
Baba Mtakatifu
anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa utoaji wa huduma
kwa: wajane, familia tenge pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi;
wengi wao wakiwa ni wale walioathirika kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Huduma hii kwa
sasa inatolewa na Kanisa kwa kusua sua kutokana na kupungua kwa misaada kutoka nje.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wafadhili wataendelea kusaidia juhudi hizi.
Baadhi
ya changamoto zinazolikabili Kanisa Katoliki Kusini mwa Afrika ni: uhaba wa miito
ya Kipadre na maisha ya kitawa; makundi makubwa ya Wakatoliki wanaokimbilia kwenye
madhehebu mengine ya Kikristo, Utoaji mimba; talaka na ndoa nyingi kuendelea kuvunjika
kiasi cha watoto kuishi katika mazingira ya wasi wasi na ukosefu wa usalama; dhuluma
na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana.
Matatizo yote haya yanahatarisha
utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; amani na utulivu ndani ya familia na jamii
katika ujumla wake. Hapa Makleri na watawa anasema Baba Mtakatifu Francisko wanapaswa
kutoa ushuhuda makini wa Mafundisho adili ya Injili, kwa kufundisha ukweli unaosindikizwa
na sala, mang'amuzi pamoja na huruma kwa wahusika.
Baba Mtakatifu amewapongeza
Maaskofu Kusini mwa Afrika kwa kuonesha mshikamano wa dhati na watu wasiokuwa na fursa
za ajira, changamoto kwa Kanisa kuwasaidia kwa hali na mali kadiri ya uwezo uliopo,
kwa kutambua kwamba, hakuna umaskini mkubwa kama ule wa kutomfahamu Kristo. Hapa kuna
haja ya kutafuta mbinu mpya ya kukutana na Kristo kwa kuwa na uelewa mkubwa wa imani.
Upungufu
wa Waseminari na Mapadre anasema Baba Mtakatifu ni changamoto kubwa katika mchakato
wa Uinjilishaji Mpya. Kuna haja ya kuhamasisha miito, kuwa makini katika kuchagua
vijana wanaotaka kuanza masomo ya Ukasisi sanjari na kuwatia moyo wa kibaba wale ambao
wako kwenye nyumba za malezi pamoja na kuwasaidia katika miaka ya kwanza kwanza baada
ya Upadrisho.
Baba Mtakatifu anaipongeza Familia ya Mungu Afrika ya Kusini
kwa kukua na kuongezeka, changamoto ya kuendelea kuziimarisha kwa njia ya Tafakari
ya kina ya Neno la Mungu, maisha ya Sala pamoja na kupokea Sakramenti za Kanisa. Waamini
wanapaswa kugundua ndani mwao umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho kama chemchemi ya
maisha ya neema.
Utakatifu na udumifu wa maisha ya ndoa ni mambo ambayo yanapaswa
kutiliwa mkazo, kwa kutambua kwamba kwa Wabatizwa, ndoa ni agano la kudumu kati ya
bwana na bibi na kwamba hii ni sadaka inayowataka wanandoa kudumisha uaminifu wao.
Maandalizi ya wanandoa watarajiwa hayana budi kukolezwa na Mafundisho juu ya Ndoa
yaliyotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo II pamoja na kuendelea kuwahamasisha vijana
kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kufunga ndoa, ili hatimaye, waweze kuwa
ni baba na mama katika familia.
Baba Mtakatifu anasema, utepetevu wa maisha
adili miongoni mwa Wakristo kwa kwa kukosa uaminifu na matokeo yake watu kujikuta
wakizama katika rushwa na ufisadi ni mambo yanayoleta athari kubwa ndani ya jamii.
Jumuiya za Kikristo zinachangamotishwa kuwa ni kielelezo cha karama ya ukweli na uaminifu,
wakisimama mbele ya Bwana wakiwa ni mikono na mioyo safi. Baba Mtakatifu anawahimiza
Maaskofu kuendelea kushughulikia matatizo mengine ya kijamii kama vile wakimbizi na
wahamiaji, ili waweze kuonja ukarimu kutoka katika Jumuiya za Wakristo.
Ni
matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mara baada ya kuadhimisha Mwaka wa Imani sanjari
na Jubilee ya miaka hamsini ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa
Kusini mwa Afrika litajielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kutangaza
kwa ari na moyo mkuu Injili ya Furaha. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa
kuiweka Familia ya Mungu Kusini mwa Afrika chini ya ulinzi na usimamizi wa Watakatifu
wa Afrika na Bikira Maria, Malkia wa Afrika awaongoze katika kufundisha, kutakatifuza
na kuwaongoza Watu wa Mungu.