Changamoto kubwa ni: Umissionari na Uinjilishaji Mpya!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano maalum na Radio
Vatican anakiri kwamba, Mwenyeheri Yohane XXIII alikuwa ni kiongozi mnyenyekevu, hodari
na shupavu, aliyethubutu kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa
kwa kuitisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Hapa Papa
Yohane XXIII akafungua malango ya Kanisa Katoliki kwa Roho Mtakatifu akapita katika
maisha na utume wa Kanisa na matunda yake, wengi wanayashuhudia wakati huu.
Askofu
mkuu Lebulu anasema, licha ya Papa Yohane Paulo II kumteuwa kuwa Askofu, alibahatika
kuwa naye karibu wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Tanzania. Wakati huo, Askofu
mkuu Lebulu, alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Hii ni hija
ambayo imeacha chapa kubwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki Tanzania. Papa
Yohane Paulo II aliwapatia maneno ya faraja na matumaini makubwa, akiwataka Maaskofu
kuwa imara katika imani, ili waweze kuwaimarisha ndugu zao katika Kristo. Kwa hakika
amekuwa ni kiongozi mashuhuri na mfano wa kuigwa katika maisha na utume wake.
Yohane
Paulo II alikuwa ni kiongozi mnyenyekevu, mwenye upendo mkubwa na aliyewajali watu
wake; akampenda Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kujitosa kimasomaso bila hata ya
kujibakiza chembe! Askofu mkuu Lebulu anasema kwamba, Kristo ndiye anayewaongoza watu
wake, lakini pia kwa mifano bora ya maisha na utume wa watakatifu, watu wengi wanavutwa
kumfuasa Kristo vizuri zaidi.
Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la
Maaskofu Katoliki anasema kwamba, changamoto kubwa na endelevu ambayo imeachwa na
Mwenyeheri Yohane Paulo II ni Umissionari na Uinjilishaji Mpya, unaojikita katika
ushuhuda wa maisha kwa njia ya imani tendaji, kama alivyofanya Yohane Paulo II wakati
wa uhai wake. Ni Kiongozi aliyetamani kuona kwamba, Kristo anawafikia watu wengi zaidi,
ili kuwaonjesha upendo na uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.
Ni Kiongozi
aliyethubutu kuwajengea uwezo waamini kumfungulia Kristo malangao ya maisha yao ili
Kristo aweze kuwapatia dira na mwongozo wa maisha. Hii ikawa kama kauli mbiu yake
katika maisha na utume wake katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Maendeleo
na ustawi wa Kanisa la Tanzania ni sehemu ya mchango wa dhati kabisa uliotolewa na
Mwenyeheri Yohane Paulo II aliyebahatika kuitembelea Tanzania na kuzungumza na watanzania
katika Majimbo makuu ya: Dar es Salaam, Songea, Tabora, Mwanza na Jimbo Katoliki la
Moshi. Maaskofu wengi ambao bado wako madarakani wakiongoza Majimbo mbali mbali nchini
Tanzania, ni matunda ya Mwenyeheri Yohane Paulo II na baadhi yao ni wale ambao wameteuliwa
hivi karibuni na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.
Ni matumaini ya Padre
Raymond Saba kwamba, Papa Francisko atawateulia Maaskofu wengine wapya ili kuziba
mapengo ya Maaskofu katika Majimbo matano ambayo hadi sasa yako wazi kutokana na sababu
mbali mbali za kichungaji.