2014-04-24 09:39:42

Watanzania wanataka Katiba ya wananchi!


Askofu Severine NiweMungizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake kwa kipindi cha Kwaresima, liliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu ukweli ambao unapaswa kuwaweka huru! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa Pasaka, likatilia mkazo ujumbe huu kwa kutoa ujumbe mwingine wa kichungaji kwa Pasaka ya Mwaka 2014 kwa kujikita katika umoja! RealAudioMP3

Askofu NiweMunguzi anasema kwamba, ukweli unaofundishwa na Yesu Kristo ukizingatiwa kwa umakini mkubwa utawafanya watu kuwa kweli huru na hivyo kuondokana na na giza pamoja na wasi wasi katika maisha ya watu. Watanzania wanaendelea kuadhimisha Kipindi cha Pasaka huku macho na masikio yao yakiwa yameelekezwa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinaendelea. Vijembe, matusi, kejeli na kususia vikao vya Bunge ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kusababisha hofu na wasi wasi kuhusu hatima ya mchakato wa Katiba Mpya nchini Tanzania.

Askofu NiweMugizi anasema, Katiba ni sheria mama inayoweka misingi ya sheria kwa sasa na kwa siku zijazo. Kipindi hiki cha Pasaka, waamini waendelee kuombea amani na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kumtuma Roho wake Mtakatifu aweze kuwaongoza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kujali mafao na ustawi wa Watanzania wote na wala si kwa makundi ya watu wala vyama vya kisiasa.

Askofu NiweMugizi anasema Watanzania wanatamani kupata Katiba ya wananchi na wala si Katiba ya Chama Tawala au Vyama vya Upinzani au hata Makundi ya watu yanayotaka kupenyeza masilahi yao binafsi. Ikiwa kama Katiba Mpya itaandikwa vyema kuzingatia mafao ya wengi, sheria nyingine zote zinaweza kupata mwelekeo sahihi kwa mfano uhuru wa kuabudu!







All the contents on this site are copyrighted ©.