2014-04-24 09:17:32

Utakatifu ni jambo linalowezekana kabisa!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maisha ya utakatifu ni jambo linalowezekana na wala si kwa ajili ya watu walioshi kanne nyingi zilizopita. RealAudioMP3

Mwenyeheri Yohane Paulo II na Yohane XXIII ni mifano hai kwamba, utakatifu unawezekana hata kwa watu wa nyakati hizi, jambo la msingi ni kumfungulia Kristo moyo wako, ili aweze kutawala na kuyaongoza maisha yako. Watakatifu ni kielelezo makini cha maisha adili na manyofu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Askofu Ngalalekumtwa anasema, alibahatika kumfahamu Papa Yohane Paulo II kunako Mwaka 1974, alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Krakovia, Poland. Alipata bahati ya kufa hija ya maisha ya kiroho wakati wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu kunako Mwaka 1975 na wakabahatika kwenda Krakovia, Poland. Walipokuwa huko kama mahujaji, Papa Yohane Paulo II alifika kuwasalimia mahali walipokuwa wanapata malazi.

Papa Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Askofu na hatimaye kumwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 6 Januari 1989 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wakati wa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania, kunako mwaka 1990, Askofu Ngalalekumtwa ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, alibahatika kuwa karibu na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II.

Alimsaidia kwa maandalizi ya Ibada kwa Lugha ya Kiswahili na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilikuwa ni kundi la mwisho kwa Mabaraza ya Maaskofu kukutana na kuzungumza na Papa Yohane Paulo II wakati wa hija za kitume zinazofanywa na Maaskofu Katoliki mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Miaka tisa baadaye, Maaskofu wanakusanyika tena mjini Vatican kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa zawadi ya utakatifu wa maisha, aliyomkirimia Mwenyeheri Yohane Paulo II ambaye walimwacha akiwa amezidiwa Hospitalini Gemelli, sasa ni Mtakatifu mbinguni, matendo makuu ya Mungu!

Askofu Ngalalekumtwa anasema, katika maisha ya ujana wake alibhatika kumfahamu Mwenyeheri Yohane XXIII na pia aliweza kushuhudia shamra shamra za maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Watakatifu hawa wawili ni kielelezo na changamoto kwa kila mwamini kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana, jaribu nawe utaona siri ya mafanikio! Kila mwamini ajitahidi kuachana na uzembe katika maisha yake kwa kujikita katika mchakato wa kutangaza Injili ya Kristo kwa uaminifu mkubwa na kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.