Sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo si sahihi kwa maendeleo ya binadamu!
Askofu mkuu Francis Chullikat, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
hivi karibuni akichangia hoja kwenye mkutano wa arobaini na saba wa Tume ya Umoja
wa Mataifa inayoshughulikia watu na maendeleo anasema kwamba, kuna haja ya kusaidia
familia ili kufikia maendeleo makubwa.
Kuna idadi
kubwa ya watu wanaoendelea kuzeeka kwa kasi na kwa upande mwingine kuna ongezeko kidogo
la watoto wanaozaliwa hususan kwenye nchi zilizoendelea zaidi duniani, hizi ni pande
mbili ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtu mzima.
Ili kuweza kuwasaidia wazee kuishi kwa amani na utulivu kuna haja ya kuwa na vijana
wa kizazi kipya wanaothubutu kujenga na kutunza familia zao, ili kuchagia pia katika
shughuli za uzalishaji na uchumi.
Askofu mkuu Chullikati anasema, inasikitisha
kuona kwamba, kuna baadhi ya Serikali zinaona mwanamke kubeba mimba kama ugonjwa unaopaswa
kupewa kinga au tiba. Hili ni jambo linalotafakarisha sana viongozi wa Seikali za
Ulaya, lakini mwono wa jumla ni kwamba ongezeko la idadi ya watu linachangia pia katika
mikakati ya maendeleo endelevu.
Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya
katika mipango ya uzazi, badala ya kudhibiti uzazi kwa sera zinazokumbatia utamaduni
wa kifo, basi, Jumuiya ya Kimataifa ijielekeze zaidi katika mikakati ya maendeleo
endelevu ya binadamu; kwa kuboresha huduma ya elimu, afya, maji sanjari na kuibua
sera ambazo ni rafiki kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia. Haya ni mambo msingi
ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo
ya mwanadamu.
Askofu mkuu Chullikati anasema, sera za haki ya uzazi salama,
kimsingi zinakumbatia utamaduni wa kifo kwa kuendekeza utoaji mimba, jambo ambalo
linakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu. Serikali zinapaswa kuwasaidia
wanawake wajawazito kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai badala ya kuwasaidia
katika mchakato wa utoaji mimba kwa njia ya sheria. Baba Mtakatifu Francisko anasema,
si mwelekeo sahihi wa kutaka kutatua matatizo ya kijamii kwa njia ya mauaji ya watoto
wasiokuwa na hatia.
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwekeza zaidi katika maboresho
ya huduma za afya, elimu, chakula na lishe bora, kwa kuheshimu na kuzingatia haki
msingi za binadamu pamoja na kuguswa na mahangaiko ya maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Sera za utoaji mimba si mkakati sahihi wa maendeleo endelevu!