Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika waanza hija ya kitume mjini Vatican
Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, SACBC, lililoanzishwa kunako Mwaka
1947 linaundwa na Nchi za Afrika ya Kusini, Bostwana na Swaziland. Maaskofu kutoka
Kusini mwa Afrika kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Aprili 2014 wako mjini Vatican
kwa ajili ya hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano.
Kanisa
Katoliki Kusini mwa Afrika linaundwa na Majimbo makuu 5 yanayoyajumuisha majimbo
20. Takwimu zinaonesha kwamba, Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki ni sawa na asilimia
kati ya 7- 8% ya idadi ya wananchi wote wa Afrika ya Kusini.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Kusini mwa Afrika kwa miaka mingi limekuwa mstari wa mbele katika mapambano
dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, demokrasia ya kweli, haki na amani. Kanisa Katoliki
limeendelea kuwa mdau mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukwimi, Kusini mwa
Afrika. Limejikita pia katika mapambano dhidi ya ukanimungu unaosababishwa na maendeleo
ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa utandawazi. Kanisa limesimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kukataa katu katu utamaduni wa kifo
na nyanyaso dhidi ya wanawake na watoto Kusini mwa Afrika.
Kanisa Katoliki
limeendelea kujielekeza katika mchakato wa kutafuta: haki, amani na upatanisho wa
kitaifa mintarafu nyaraza ya Sinodi za Afrika pamoja na kujikita katika Uinjilishaji
Mpya, unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini kutolea ushuhuda wa imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake, kama chachu ya kuyatakatifuza malimwengu pamoja na kumhudumia
mtu mzima katika mahitaji yake msingi. Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu wa kuwa
na demokrasia ya kweli pamoja na kusimamia ustawi na mafao ya wengi; ukweli na uwazi,
nidhamu na uwajibikaji.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, Alhamisi
tarehe 24 Aprili 2014 linakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.