Kwa njia ya kazi mwanadamu anashiriki kazi ya uumbaji na ukombozi
Karol Jozef (Yozef) Wojtyla alizaliwa tarehe 18 Mei 1920 mjini Wadowice karibu na
mji wa Krakovia kusini mwa nchi ya Poland, na alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watoto
watatu. Kwa bahati mbaya , hakubahatika kuwafahamu ndugu zake, kwani walifariki dunia
kabla ya yeye kuzaliwa.
Akiwa na umri
wa miaka tisa (9), mama yake alifariki dunia na kumuacha mtoto huyo akilelewa na baba
yake, ambaye pia alifariki dunia wakati Karol akiwa na umri wa miaka 21, mnamo mwaka
1941. Mazingira ya kijamii alimokulia Karol: mnamo mwaka 1939 Vita vya Pili vya Dunia
vilikuwa tayari vimekwisha anza na nchi yake ilivamiwa na Wajermani mnamo mwaka 1939,
na kipindi hicho chicho nchi hiyo pia ilichukuliwa na Wakomunisti.
Katika
kipindi hiki cha vita, kijana Karol alifanya kazi kama mhudumu wa hoteli ili kuweza
kujiendeleza na masomo yake. Kuanzia mwaka wa 1940, kwa takriban miaka minne, Karol
alisoma kwenye seminari ya kificho (kutokana na kwamba wakomunisti walifunga na kukataza
maeneo ya ibada na seminari zilitekwa), na mnamo tarehe mosi Nov.1946 akapata daraja
la upadre. Aliteuliwa kuwa Askofu mnamo mwaka 1958; akateuliwa kuwa Kardinali wa Jimbo
kuu la Krakovia mnamo mwaka 1967; mnamo tarehe 16 Oktoba 1978 akachaguliwa kuliongoza
Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hadi Mwenyezi Mungu alipomwita kwenye
makao ya milele mnamo tarehe 2 Aprili 2005.
Mchango wake katika kuendeleza
mafundisho jamii ya Kanisa ulijidhihirisha wazi katika mahubiri yake aliyotoa kwenye
mahubiri ya misa yake ya kwanza kama papa aliposimikwa rasmi kuliongoza Kanisa Katoliki.
Mchango huo unajisìdhihirisha kwenye mahubiri yake alipowaambia waumini wa Kanisa
katoliki na wale wote waliokuwa wamekusanyika kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la mtakatifu
Petro mjini Vatican: Ndugu zangu, msiwe na hofu ya kumkaribisha Kristo na kukubali
mamlaka yake. Na kwa uwezo wa mamlaka ya Kristo mumtumikie mwanadamu na ulimwengu
mzima. Msiogope. Mfungulieni Kristo milango ya mioyo yenu, kwani ndiye pekee anayejua
kile kilichopo ndani ya moyo wa mwandamu. Ni Kristo tu anayejua. Mruhusuni Kristo
aongee ndani ya mioyo yenu na ndani ya moyo wa kila mwanadamu. Kwa kupokea mamlaka
yatokayo kwa Kristo, Papa Yohane Paulo II aliweza kuongea na moyo wa kila mwanadamu
kwa njia ya mafundisho aliyoyatoa kama kiongozi wa Kanisa, na mchango wake katika
kukabiliana na hali halisi ilivyokuwa kikanisa, kijamii na kimataifa wakati akiwa
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Alitoa mchango wake katika jamii kwa njia ya nyaraka
mbili zilizohusu mafundisho jamii ya kanisa, ambazo ni Laborem Exercens (Kazi ya
mikono ya mwanadamu), na Solicitudo Rei Socialis (Kuhusu maswala ya jamii).
Tunaweza
kujiuliza kwamba, ni kwanini papa aandike waraka kuhusu kazi ya mikono ya mwanadamu,
au kuhusu maswala ya jamii? Ili kuelewa nyaraka hizi vizuri, tunapaswa kufanya rejea,
walau kwa kifupi tu kuhusu hali halisi ilivyokuwa kimataifa wakati papa alipochaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki. Tuko kwenye kipindi cha miaka ya 1980. Uchumi wa nchi
tajiri umeendela kukua kutokana na mapinduzi ya viwanda na maboresho ya teknolojia
kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kwa wingi kwa kutumia mashine, na hivyo, kupunguza
pia ajira kwa kazi zilizokuwa zikifanywa kwa mikono kwani haikuwa tena na sababu.
Laborem Exercens ilichapishwa mnamo tarehe 14 Septemba 1981, kwanza kabisa
kwa lengo la kuadhimisha miaka 90 ya waraka wa kwanza wa kijamii ulioandikwa na papa
Leo XIII, Rerum Novarum, mnamo mwaka 1891, ambao mapapa wote waliofuata waliendelea
na wanaendelea kuutumia kama rejea katika kuendeleza mafundisho jamii ya Kanisa. Pili,
Laborem Exercens iliandikwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko makubwa ya kijamii
yaliyoikumba dunia tangu Mapinduzi ya Viwanda yalipotokea katika nchi za Ulaya na
Marekani, mapinduzi ambayo yalileta pia athari kwenye uelewa wa hadhi na haki za
wafanyakazi.
Papa Yohane Paulo II anabainisha baadhi ya mabadiliko haya na
athari zake katika ulimwengu wa ajira na, mabadiliko ambayo yalihitaji marekebisho
kwenye miundo ya uchumi na utoaji wa ajira.Mabadiliko haya yanahusu: maendeleo ya
sayansi na teknolojia na ueneaji wa mashine za kuzalishia bidhaa viwandani, kuongezeka
kwa gharama za nishati na malighafi, uhaba wa rasilimali ya dunia, na uelewa juu
ya uharibifu wa mazingira. Vile vile, LE iliandikwa kwa ajili ya kukabiliana na uelewa
hasi juu ya maana ya kazi na upungufu wa maadili katika ulimwengu mamboleo.
Katika
kuongelea swala la kazi, mwanadamu anapewa kipaumbele cha pekee kwani kazi inayo hadhi
yake, na hadhi hiyo inatokana na kwamba kazi inafanywa na mwandamu. Katika waraka
huu, papa yohane Paulo II anasisistiza kwamba, kwa njia ya kufanya kazi, au kwa njia
ya kazi, mwanadamu anaendeleza kazi ya uumbaji ambao tayari Mungu aliuanza. Kwa hiyo,
kadiri ya mafundisho ya papa juu ya kazi, ni kwamba kitu cha kuthamini si kazi kama
kazi bali ni mwanadamu anayefanya kazi na ambaye anaipatia maana kwa utu na utendaji
wake. Vilevile , kazi inampatia mtu hadhi katika maana kwamba, pale mtu anapofanya
kazi na kuzalisha, anaweza kukidhi mahitaji yake binafsi na mahitaji ya wale ambao
wako chini ya ulinzi na usimamizi wake.
Mambo yanapofanyika kinyume na hivi,
matokeo yake ni mtu kuchukuliwa kama mojawapo ya vyombo vya kuzalishia faida inayotokana
na kazi, au hata kuuzwa kama bidhaa. Hali hii ina kuudhalilisha utu wa mtu, jambo
ambalo halikubaliki machoni pa mwenyezi Mungu. Ili kuweza kuondokana na nayanyaso
ambazo wafanyakazi wanaweza kukumbana nazo, papa anatoa ushauri kwamba wafanyakazi
waunde vyama vya ushirika wa wafanyakazi ili kwa pamoja na kwa mshikamano waweze kuwa
na nguvu ya kudai haki zao ambapo haziheshimiwi. Vyama hivi, kadiri ya mafundisho
ya Papa Yohane Paulo II vitasaidia pia katika kupata haki katika jamii.
Kanisa
Katoliki katika Mafundisho yake Jamii daima limetoa kipaumbele cha pekee kwa mwanadamu.
Kutokana na ukweli kwamba kazi ni tendo linalo pata chumbuko katika utashi wa mwanadamu,
kinachofuata ni kwamba, mwanadamu anashiriki katika kazi kwa hali zake zote kiroho
na kimwili. Kwa maana hiyo, Kanisa linao wajibu na jukumu la kuwaelewesha watu kuhusu
thamani ya kazi na maadili yanayopaswa kuambatana nayo na kwa njia hii kuonesha taalimungu
iliyopo kwenye kazi. kusema kwamba kazi pia inayo tasaufi yake ina maanisha kwamba
kwa njia ya kufanya kazi kwa uadilifu mwanadamu anaweza pia kuishi katika muunganiko
na Mungu na kukuza urafiki na Yesu Kristo mkombozi wa dunia, na hivi kuendeleza ule
mpango wa ukombozi ulioletwa na Mungu mwenyewe. Papa Yohane Paulo II katika waraka
huu anashauri kwamba maisha ya kiroho hayahusu tu sala, tafakari, kusifu na kuabudu,
au mambo mengine kama hayo, bali pia maisha ya kiroho yanaweza kuhusisha pia kazi.
Hapa ina maanisha kwamba, ikiwa mtu katika utendaji wake wa kazi yoyote halali,
anaifanya si tu kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe bali pia kwa ajili ya kuwasaidia
wengine na kwa nia ya kuendeleza kazi ya uumbaji wa Mungu, hata hapa kuna uhusiano
kati ya kazi na maisha ya kiroho.
Waraka huu unatoa mtizamo mpy wa maisha
ya kiroho na unatualika sote tuondokane na ile dhana ya kuelewa maisha ya kiroho kama
hali ya kujikatalia na kuenzi dhana nyingine ambayo ni maisha ya kiroho yanayo mfanya
mtu awajibike mbele ya jamii na kwenye jamii, bila kuaiacha safari yake ya kiroho.
Kazi ni wito ambao mwanadamu ameitiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu, pale Mungu alipomwambia
Adamu kwamba atapata chakula chake kwa njia ya jasho la uso wake, yaani kwa njia
ya kazi.
Kupata chakula kwa njia ya jasho kuna maanisha kuchoka, na hata kupoteza
nguvu za mwili kwa namna moja au nyingine, na hii inaweza kuonekana kama sehemu hasi
ya kazi. sehemu chanya ni ile inayotokana na kwamba, kwa njia ya kazi mwanadamu anashiriki
kazi ya uumbaji na anaiendeleza, na kwa kuiendeleza anajipatia pia kipato chake kinachomfanya
aishi katika maisha yenye hadhi kwenye jamii na kuwawezesha wengine kuishi maisha
yenye hadhi. Ila hata katika sehemu hasi ya kazi, ambayo ni mchoko, Papa Yohane Paulo
II alitufundisha kuipa thamani. Anasema, uchovu na shida zinazotokana na kazi vinaweza
kuwa na thamani ikiwa mwanadamu, na hasa mkristo, ataviunganisha na mateso ya Kristo.
Papa
anafundisha kwamba “ kwa njia ya uvumillvu wa uchovu unaotokana na kazi, na kwa kuunganisha
uchovu huo na mateso ya Kristo aliyesulibiwa kwa ajili yetu, mwanadamu anashirikiana
na mwana wa Mungu katika kazi ya kuuokomboa ulimwengu. Hivyo basi, kwa namna hii
tunaweza kusema kwamba, mafundisho ya Papa Yohane Paulo II kuhusu kazi ni kwamba,
kwa njia ya kazi mwanadamu anashirki katika uumbaji na ukombozi wa ulimwengu. Imeandaliwa
na Sr. Gisela Upendo Msuya, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Toma wa Akwino, Angelicum,
Roma.