Wanawake simameni kidete kutetea Injili ya Uhai, msikubali kukumbatia utamaduni wa
kifo!
Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anawahamasisha
wanawake kuwa ni watetezi wakuu wa Injili ya uhai badala ya kukumbatia utamaduni wa
kifo, unaojikita katika sera za utoaji mimba na mpango wa uzazi, unaowanyima watoto
fursa ya kuzaliwa kwenye familia. Kardinali Pengo amewataka wanawake na wasichana
kukuza dhamiri nyofu kwa kuheshimu Amri za Mungu na Mafundisho Kanisa.
Kardinali
Pengo ameyasema hayo, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, Jumatatu ya Pasaka, iliyowaunganisha
waimbaji wa Shirikisho la Kwaya Jimbo Kuu la Dar es Salaamili kusherehekea Siku kuu
ya Pasaka pamoja. Wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko ndani ya Jamii,
kwa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu, kumbe kuna haja kwa wanawake
na wasichana kufundwa sawasawa, ili waweze kuwa na dhamiri nyofu, itakayowasaidia
kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba
tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu
Kardinali
Polycarp Pengo amekemea pia tabia ya baadhi ya watu kudai haki ya kuwa na ndoa za
watu wa jinsia moja, kwamba ni jambo linalokiuka Amri za Mungu, maadili na utu wema.