2014-04-22 08:23:10

Papa Yohane XXIII alisimamia: Amani, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Umoja wa Wakristo


Waraka huu wa Pacem in Terris, Amani Duniani ni waraka wa pili wa kijamii wa papa Yohane XXIII. Waraka huu ulionekana kwa baadhi ya watu kama ndoto ya mchana ya papa Johane wa XXIII kwani ulitolewa muda mfupi tu baada ya nchi ya Cuba kurusha makombora yake ambayo yaliiacha dunia ikiwa katika hofu kubwa ya kuzuka vita vya nyuklia kati ya Marekani na Urusi. RealAudioMP3

Papa Yohane wa XXIII alisema kuwa Waraka wake huu wa pili kuhusu jamii alikuwa anauelekeza kwenye jumuiya ya kimataifa, jumuiya ambamo, kila mtu angali anatambua haki zake binafs na wajibu alionao katika jamii, atajibiddisha kutenda kwa kufuata misingi yausawa na amani na hivi kuchangia katika kukuza yake mambo yaliyo na mafao kwa watu wote kuliko kuongozwa na ubinafsi.

Jinsi hali ilivyokuwa duniani wakati waraka huu unatolewa kunako Mwaka 1962: Vita baridi kati ya Marekani na Urusi ilikuwa inapamba moto. Mwezi machi mwka huohuo, ukuta wa Berlin ukapanda juu. Kwenye mwezi wa kumi mwaka huo huo, muda mfupi tu baada ya Mtaguso kuanza Marekani na Urusi wanatishiana kuanzisha vita vya nyuklia kutokana na Urusi kuweka makombora yake huko Cuba.

Hali hii iliwalazimu wakuu wa Vatican kusitisha mkutano na kuwaruhus maaskofu kurudi majimboni mwao kutokana na hali tete iliyokuwepo na ambayo hatma yake haikuwa inaeleweka wala kujulikana. Kwenye nchi za kikomunisti serikali zilikuwa zikiwatesa wakatoliki na mapadre wengi pamoja na maaskofu walitiwa magerezani.

Katika hali kama hii, papa alitoka kifua mbele na kujaribu kufanya mazungumzo na viongozi husika ambao walikuwa na uwezo pia wa kisitisha vita ambayo ingeleta madhara ulimwenguni kote na si tu kwenye nchi hizi mbili. Katika kipindi hiki papa alifaulu kuwashawishi viongozi hawa wawili kuweka chuki zao pembeni na kuangalia manufaa ya ulimwengu mzima. Wakati wa misigano hii ya kivita na kwenye kipindi cha miezi michache aliyokuwa nayo bado ya kuishi, papa aliishawishi jumuiya ya kimataifa kutatua migogoro kwa njia ya majadiliano na makubaliano badala ya kukimbilia vita kama suluhu ya migogoro ya kijamii.

Anasisitiza kwamba kila mwanadamu anapaswa kufanya kila linalowezekana ili kujenga, kulinda na kudumisha amani duniani. Kwa ari ya utumishi aliyokuwa nayo, hakusita kuongea na marais wa mataifa makubwa ambaoo wakiluwa na wajibu wa kuilinda amani duniani, nao walimsikiliza na kumtii. Hapo dunia ikaokolea kutokutumbukia kwenye vita ya nyuklia.

Mwezi mmoja baada ya mapambano hayo mazito, yaani tarehe 16 Novemba 1962, Papa anaambiwa na daktari wake kwamba amepata ugonjwa wa Saratani na kwamba, alikuwa na muda mfupi tu wa maisha. Na kweli miezi sita baadaye papa Yohane wa XXIII akaaga dunia mnamo tarehe 3 Juni 1963. Juma moja kabla ya kufariki dunia, mbele ya waliokuwa wasaidizi wake wa karibu kwa kipindi kile, alikiri tena nia yake ya kulitumikia Kanisa kama mtumishi wa familia ya mwanadamu. Aliwaambia wasaidizi wake “ sasa kuliko nyakati zingine zote, tunaitwa kumtumikia mwanadamu na binadamu wote, si tu Wakatoliki; tunaitwa kutetea kwanza kabisa na kila mahali haki za binadamu na si tu haki za Kanisa Katoliki.

Hivi ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Papa Yohane kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Pamoja na magumu yote aliyokumbana nayo katika hali ya kanisa la kidunia na mazingira ya kisiasa na kiuchumi, bado hakusita kufundisha kwamba Kanisa ni Mama na Mwalimu, kwani limetuzaa kwa njia ya sakramenti, na linatufundisha na kutuelekeza njia ya kumfikia bwana na muumba wetu. Vilevile akasisitizia kwamba, amani duniani inahitaji mchango wa kila mwanadamu katika kuitafuta, kuilinda na kuitetea.

Kwa kipindi cha muda mfupi, kutokana na nguvu ya hadhi yake, maneno na matendo yake, Papa Yohane wa XXIII alileta mabadiliko makubwa ndani ya Kanisa Katoliki kwa kulisaidia kubadili mwelekeo kutoka jinsi ambavyo lilikuwa likijiweka na kueleweka na ulimwengu, na kuwa na sura mpya. Mchango wake uliwashangaza wale waliokuwa wakilitazama kanisa kwa mbali na ambao hawakuwa na matarajio makubwa kutoka kwa papa huyu aliyeonekana mwenye kimo kifupi na mwenye asili ya kikulima.

Hata yeye alijua kwamba watu wengi hawakuwa na matarajio makubwa kutoka kwake, lakini aliwashangaza baadaye pale aliposema “ kila mtu aliamini kwamba mimi ningekuwa Papa wa mpito na ambaye hangefanya chochote ndani ya Kanisa. Ila bado niko hapa, ninatimiza miaka minne ya utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro nikiwa na ratiba nzito ya kazi za kichungaji ambayo iko mblele yangu na ambayo napaswa kuitekeleza mbele ya uso wa dunia ambao unaangalia na kusubiri”. Ratiba hii nzito ya kazi ya kichungaji ilikuwa ni ile ya kuitisha Mtaguso Mkuu wa Kiuekumene.

Matukio haya makuu matatu ya kipindi cha Yohane wa XXIII yalikuwa sehemu ya mtizamo wake wa kiuchungaji. Kila moja ya matukio haya lilikuwa na nguvu ya pekee katika maisha na utume wa papa, na pia kila moja ya matukio haya lilitoa mwelekezo kuhusu mtizamo ambao kanisa lilipaswa kuwa nao kuhusu maswala ya jamii na ulimwengu kwa ujumla. Kwa namna moja au nyingine, tunaweza kusema kwamba papa Yohane wa XXIII alilipatia kanisa utambulisho mpya katika ulimwengu.
Alifika mahali akagundua kwamba, mtizamo aliotaka kanisa liwe nao haungeonekana wakati wa utume wake kama Khalifa wa mtakatifu Petro. Pamoja na hayo, alitumia nguvu zake zote na utashi wake kwa ajili ya kutekeleza swala hili. Akiwa mgonjwa mahututi kitandani mwake karibu na kukata roho alitoa kauli ifuatayo: “kitanda hiki ni madhabahu. Madhabahu yanahitaji kafara (sadaka). Nami niko tayari kujitoa kama kafara. Ninayatoa maisha yangu kwa ajili ya Kanisa, kwa ajili ya mwendelezo wa Mtaguso Mkuu wa kiekumene, kwa ajili ya amani duniani na kw ajili ya Umoja wa Wakristo”. Aliaga dunia na kurudi kwenye makao ya Baba wa mbinguni mnamo tarehe 3 Juni 1963.

Imeandaliwa na
Sr. Gisela Upendo Msuya,
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Toma wa Akwino,
Angelicum, Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.