2014-04-22 10:15:35

Mwanga wa Pasaka na matumaini ya wananchi wa Syria!


Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko "Urbi et Orbi" kwa ajili ya mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, wakati wa Siku kuu ya Pasaka, umegusia kwa namna ya pekee mahangaiko na mateso ya wananchi wa Syria kwa kutoa mwaliko kwa pande zinazohusika kujikita katika majadiliano ya amani pamoja na kuruhusu wananchi wanaoteseka kupata msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa.

Huu ni ujumbe ambao umeamsha kwa mara nyingine tena matumaini ya wananchi wa Syria na kwamba, huu ni wajibu wa kimaadili unaopaswa kutekelezwa na viongozi wa kisiasa, ili amani ya kweli iweze kupatikana. Ni maneno ya Askofu mkuu Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Syria, katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka huu. Imekuwa ni Siku kuu inayoonesha umoja na mshikamano miongoni mwa Makanisa pamoja na faraja kwa watu wanaoteseka, ambao kimsingi bado wamebaki "Ijumaa kuu" kutokana na vita mahangaiko ya maisha.

Askofu mkuu Zenari anasema, watu wengi kwa sasa wanakabiliwa na baa la njaa, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia juhudi za upatikanaji wa chakula cha msaada pamoja na ulinzi, ili msaada huu uweze kuwafikia walengwa. Bado kuna watu waliotekwa nyara ambao hawajulikani mahali walipo. Ni mwaka mmoja tangu Padre Paolo Dall'Oglio alipotekwa nyara; wote hawa wanasubiri siku moja kuona Mwanga wa Kristo Mfufuka.







All the contents on this site are copyrighted ©.