2014-04-22 16:32:03

Msishabikie uvunjifu wa amani na utulivu!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi nchini kuacha kuwatumia wananchi kama chambo cha kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kusababisha migororo na uvunjifu wa amani.

Aidha, Rais Kikwete amewataka wananchi wa Wilaya ya Karatu wasiige mfano wa Arusha ambako fujo zinazoongozwa na baadhi ya viongozi zimezorotesha sana uchumi wa mji huo kwa sababu usalama ni kigezo kikuu cha maendeleo ya uchumi.

Akizungumza wakati anazindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, mjini Karatu asubuhi ya leo, Jumanne, Aprili 22, 2014, Rais Kikwete amesema: “Usalama ni jambo muhimu sana na kwa maana hiyo, nawaombeni msiige kabisa mfano wa Arusha, sote tunajua kimetokea nini kule kwa sababu ya fujo za kisiasa ambazo zinachochewa na viongozi na hasa Mbunge wa Arusha mjini Bwana Lema,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Mbunge anayo nafasi kubwa kujenga hoja zake ndani ya Bunge na ndani ya mikutano ya halmashauri. Lakini kwa mbunge kuwachochea wananchi na kuwachukua na kuwatembeza barabarani ambako wanakumbana na virugu vya polisi siyo uongozi wa busara hata kidogo.”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Mheshimiwa Lazaro Titus Massey amewaambia wananchi kuwa moja ya mwelekeo mkuu wa CHADEMA wilayani Karatu ni kushirikiana na Serikali na polisi katika kudumisha amani. Tunawakaribisha Arusha waje kujifunza kwetu namna ya kudumisha amani. Tunamkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Bwana John Mongella kuja kujifunza namna ya kurejesha na kudumisha amani mjini humo.

Tutaendelea kutumia mashine mpya kukusanya kodi – Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Mashine za Electroniki za Ukusanyaji Kodi –EFD ni lazima ziendelee kutumika nchini na ameagiza viongozi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kukaa chini na wadau na watumiaji wa mashine hizo kuzungumza na kutafuta majawabu yanayolalamikiwa na wadau.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa anajua kuwa yapo maneno mengi kuhusiana na mashine hizo lakini Serikali haitarudi nyuma katika matumizi ya mashine kwa sababu dunia nzima inakwenda huko. Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali kuhusu EFD, Jumanne, Aprili 22, 2014 wakati alipozunguza kwenye sherehe ya uzinduzi wa Ofisi za TRA mjini Karatu, Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha.

“Najua kuna maneno mengi kuhusu suala hili. Kwa hiyo maelekezo yangu ni kwamba kaeni chini, myajadili matatizo yaliyopo na kupata ufumbuzi. Kama ni suala la bei pia linazungumzika lakini tuhajitaji mfumo huu wa malipo ya kodi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kwenye hili tusirudi nyuma kwa sababu tukifanya hivyo, tutakuwa
tunarudi nyuma sana kwa sababu dunia nzima inaelekea huko na hata majirani zetu wote ama wameanzisha mfumo huo ama wanajiandaa kuuanzisha.” Rais Kikwete amesisitiza: “Hatuwezi kurejea kwenye mfumo ule wa kitumia vijirisiti. Mfumo wa sasa unaifanya kazi ya kukusanya kodi kuwa rahisi kwa Serikali yenyewe na kwa walipa kodi.

Najua watu hawapendi kulipa kodi lakini hakuna njia ya jinsi ya kuendelea isipokuwa kwa kulipa kodi”. Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya siku moja kukagua shughuli za maendeleo wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kesho atafanya ziara kama hiyo ya siku moja katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.








All the contents on this site are copyrighted ©.