Mwanga wa Kristo mfufuka ulete furaha, faraja na matumaini!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2014 wakati wa Sala
ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican,
ameendelea kuwatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kheri na baraka kwa Siku
kuu ya Pasaka, kwani hii ndiyo Siku aliyoifanya Bwana, chemchemi ya furaha na matumaini
mapya hata kwa mitume wa Yesu waliopashwa habari kwamba, hakika Yesu amefufuka, changamoto
na mwaliko kwa waamini kuacha chapa hii ya Injili kujikita katika mioyo na maisha
yao yote!
Baba Mtakatifu anasema mwanga huu hauna budi kwanza kabisa kububujika
kutoka katika undani wa moyo wa mtu mwenyewe, kama ilivyokuwa kwa Magdalena, aliyekuwa
analia kwa kumkosa Yesu na kwamba, macho yake hayakuamini alipokutana uso kwa uso
na Kristo Mfufuka, kiasi kwamba, amekuwa ni shahidi wa Kristo Mfufuka, chanzo cha
maisha mapya na mwaliko wa kupeleka mwali wa Kristo mfufuka katika medani mbali mbali
za maisha ya watu: kwa watu wenye furaha waweze kuwa na furaha zaidi kwa kuwaondolea
ubinafsi na wale wanaoteseka na kuhuzunika wapate faraja na matumaini mapya.
Baba
Mtakatifu anasema, Bikira Maria aliteseka sana pale upanga wa huzuni ulipopenya moyoni
mwake, lakini furaha ya kufufuka kwa Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, ilikuwa ni kubwa
kiasi kwamba, mitume waliweza kuchota furaha hii kutoka kwa Bikira Maria. Mateso,
kifo na ufufuko wa Kristo ni kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa Mungu, kiasi
kwamba, Moyo Mtakatifu wa Bikira Maria umekuwa ni chemchemi ya: amani, faraja, matumaini
na huruma. Ukuu wa Bikira Maria unapata utimilifu wake kwa kushiriki katika Pasaka
ya Kristo, daima ameendelea kuwa ni Mama wa mateso na matumaini; Mama wa mitume na
Kanisa.
Bikira Maria ni shahidi wa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia katika Kipindi hiki cha Pasaka ili kuwashirikisha
furaha ya Pasaka. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia waamini, mahujaji na wageni
wote waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican furaha
ya Kristo Mfufuka.