2014-04-21 10:29:28

Bado kuna watu wana mashaka kama Mtakatifu Toma!


Askofu Munib Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Nchi Takatifu na Yordan katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pasaka anawataka wananchi wa Israeli na Palestina kujenga matumaini ya kuweza kuishi kwa pamoja katika misingi ya haki, amani na utulivu pamoja na kuondokana na mashaka na wasi wasi, ambao umekuwa ni sehemu ya historia ya maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Hii inaonesha kwamba, hali ya kutoaminiana inaendelea kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, aliyetia mashaka kuhusu ufufuko wa Yesu. Wananchi walioko huko Mashariki ya Kati wanaendelea kuhoji ikiwa kama mchakato wa kutafuta suluhu ya amani utapata muafaka, watu wameshikwa na wasi wasi kuhusu vita na uvamizi; nyanyaso na dhuluma pamoja na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Watu wana imani haba kama kiatu cha raba, kiasi hata cha kuhoji uwepo wa Mungu katika maisha yao! Hii ni kutokana na kushamiri kwa vitendo ambavyo vinakwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu.

Katika ulimwengu mamboleo, bado kuna watu wanaotaka kuhakiki kila jambo kama alivyofanya Mtakatifu Toma. Kwa watu wenye mashaka wanageuza matumaini yao kwa viongozi wakuu wa Mataifa ili waweze kuwasaidia kuvuka vikwazo vya kiuchumi na matumizi ya nguvu. Askofu Munib Younan anasema kwamba, Yesu alimfundisha Mtakatifu Toma kuwa na imani na matumaini hata pale mambo yote yanapoonekana kukosa mwelekeo.

Ufufuko wa Kristo ni tukio kubwa linaloshinda mashaka na wasi wasi; nguvu ya watawala wa dunia hii; dhuluma, ukatili na misimamo mikali ya kiimani. Yesu anaweza kuleta mwelekeo mpya wa historia ya maisha ya mwanadamu, ikiwa kama watamtumainia bila mashaka!







All the contents on this site are copyrighted ©.