2014-04-21 10:19:52

Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele kuzikwa Jimbo kuu la Mombasa 22 Aprili 2014


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA linaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kwa namna ya pekee na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa kuomboleza kifo cha Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele, Jimbo kuu la Mombasa kilichotokea hivi karibuni huko Mombasa kutokana na ugonjwa wa moyo. RealAudioMP3

Askofu mkuu Tarcisio Zizaye, Mwenyekiti wa AMECEA katika ujumbe wake, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu aliomtendea Marehemu Askofu mkuu mstaafu Lele katika maisha na utume. AMECEA itamkumbuka sana kutokana na huduma makini aliyoifanya kwa Familia ya Mungu nchini Kenya kama Padre, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kitui na hatimaye, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mombasa.

Askofu Anthony Mueria wa Jimbo Katoliki Kitui, Kenya anasema, wamepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele, aliyewahi kuwa Askofu wa Jimbo la Kitui, kwa masikitiko makubwa, kwani Askofu mkuu Lele ni kati ya Mapadre wa kwanza kabisa kutoka Jimbo Katoliki la Kitui. Kwa Familia ya Mungu Jimboni humo, amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na Mapadre, Watawa na Waamini katika ujumla wao.

Marehemu Askofu mkuu Boniface Lele alizaliwa kunako tarehe 14 Aprili 1947, Kitui, Mashariki mwa Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 8 Desemba 1974. Kunako tarehe 2 Februari 1996 akateuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kitui.

Tarehe 1 Aprili 2005 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mombasa alikotumikia kwa moyo mkuu hadi tarehe 1 Novemba 2013 alipong’atuka kutoka madarakani kutokana na sababu za afya. Taarifa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya zinaonesha kwamba, Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele atazikwa tarehe 22 Aprili 2014 kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Mombasa. Ibada hii inatarajiwa kuanza majira ya saa 4: 00 Asubuhi.

Maiti ya Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele inatarajiwa kutolewa kwenye Hospitali ya Pandya, jioni tarehe 21 Aprili 2014, ili kutoa nafasi kwa Familia ya Mungu nchini Kenya kukesha na kuomboleza. Watu wengi wataendelea kumkumbuka Marehemu Askofu mkuu mstaafu Lele kutokana na unyofu wake na bidii katika kuwahudumia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hakutakuwa na uwekaji wa mashada ya maua na badala yake, wale wanaotaka kununua mashada ya maua wanaweza kutoa sadaka na mchango wao kusaidia maskini Jimbo kuu la Mombasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.