Zawadi ya Pasaka kutoka kwa Papa Francisko kwa maskini wa mji wa Roma!
Askofu mkuu Konrad Krajewski,Mtunza sadaka ya Papa katika maadhimisho ya Siku kuu
ya Pasaka kwa Mwaka 2014 amewatembelea maskini wa mji wa Roma na kuwapatia zawadi
ya Pasaka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hawa ni watu wanaoishi katika maeneo
ya vituo vikuu vya reli, eneo la Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu mjini Roma pamoja
na Ostiense.
Zawadi ya Baba Mtakatifu kwa maskini ni mchango unaotolewa na
waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanapoomba vyeti vya baraka kutoka kwa Baba
Mtakatifu. Zawadi na ukarimu wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha Kwaresima
imewafikia pia wanawake 30 wanaotunzwa na Masista wa Mama Theresa wa Calcutta.
Askofu
mkuu Krajewski anasema, Baba Mtakatifu Francisko alipomteuwa kuwa Askofu mkuu na mtunza
sadaka wake, alimtaka kumsaidia kuwafariji maskini na kamwe asijenge mazoea ya kukaa
ofisini na kwamba, mahubiri ya Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa
amekazia umuhimu wa kutumia fedha kwa busara na kamwe watu wasitawaliwe na uchu wa
mali kwani matokeo yake ni mabaya katika maisha ya watu.