2014-04-20 08:16:23

Watu wamechoka na vita wanataka amani na utulivu!


Shirikisho la Baraza ya Makanisa Sudan ya Kusini linasema kwamba, hakuna matumaini ya kesho iliyo bora zaidi kwa wananchi wa Sudan ya Kusini, ikiwa kama wahusika wakuu wa vita na mgogoro wa kijamii hawatasitisha mashambulizi na kuanza mchakato wa upatanisho, haki, amani na maendeleo. Vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Sudan ya Kusini ina madhara makubwa kwa watu na maendeleo yao.

Shirikisho hili linarudia tena kutoa wito kwa Serikali na wapinzani kusitisha mara moja vita na kinzani za kijamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wananchi wa Sudan ya Kusini, badala ya kuelemewa na uchu wa mali na madaraka ambao umekuwa ni chanzo kikuu cha majanga na mateso ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Viongozi wa Makanisa wanawataka wahusika wakuu katika mgogoro wa kivita nchini Sudan ya Kusini kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita yaliyotiwa sahihi mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Ni mwaliko pia kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia juhudi hizi ili mkataba huo uweze kuheshimiwa na pande zote mbili. Vita inayoendelea nchini Sudan ya Kusini imekwisha sababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Wananchi wa Sudan ya Kusini walipiga kura ya maoni na kushinda wakitamani kuwa na Nchi huru, inayoongozwa katika misingi ya haki, amani, utu na usawa. Watu wana kiu ya amani ya kudumu, itakayosaidia kukoleza mchakato wa maendeleo yao na wala si vita inayojikita katika uchu wa mali na madaraka!







All the contents on this site are copyrighted ©.