Msalaba wa Kristo unafumbata: upendo, huruma na msamaha!
Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo wakati wa Ijumaa kuu, ilikuwa
ni nafasi kwa Mama Kanisa kuangalia sura ya Kristo katika mateso na mahangaiko ya
watu wake. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Njia ya Msalaba alisema
kwamba, Yesu amebeba dhambi za binadamu katika mabega yake na kwamba, usaliti wa Yuda
na Petro uliongeza uzito wa Msalaba. Huu ndio uzito wa Msalaba unaojionesha kwa watu
wanaoishi katika upweke hasi, dalili za kifo; kifo kwa ndugu na jamaa pamoja na uwepo
wa dhambi!
Msalaba ni kielelezo cha upendo, utukufu na huruma ya Mungu kwa
binadamu ambaye kamwe, hawatendei watu wake kadiri ya dhambi zao, lakini kadiri ya
huruma na upendo wake. Kwa njia ya mateso ya Kristo Msalabani, mwanadamu anaonja upendo
wa Kristo na tumaini la maisha mapya.
Mwanadamu daima yuko katika hija ya
maisha ambayo hatima yake ni kifo, lakini kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Yesu ameshinda
kifo na dhambi na kwamba, upendo, huruma na msamaha wa Mungu ni mambo msingi katika
hija ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia Kristo
katika mateso yake, ili waweze kufufuka pamoja naye.