2014-04-19 07:40:24

Matashi mema ya Pasaka kutoka kwa Jumuiya ya Wayahudi wa Roma kwa Papa Francisko


Rabbi mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma Riccardo di Segni amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema wakati huu Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Pasaka. Anasema, mwingiliano wa Siku kuu hizi mbili yaani Pasaka ya Wayahudi, "Pesach" na Pasaka ya Wakristo ni mwaliko wa kutazama tunu msingi zinazowaunganisha kwa pamoja, hususan imani kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu anayeongoza historia ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa na kumdhaminisha mwanadamu kazi hii nyeti.

Rabbi mkuu Riccardo di Segni anasema, kutangazwa kwa Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu ni kuonesha mchango mkubwa uliotolewa na Mapapa hawa wawili katika historia inayoonesha mabadiliko makubwa na yenye mwelekeo chanya katika mahusiano kati ya Wayahudi na Kanisa. Hili ni tukio la matumaini kwa wote.

Mwishoni mwa ujumbe wake wa Pasaka kwa Baba Mtakatifu Rabbi Riccardo di Segni anagusia pia hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko inayotarajiwa kufanyika Mwezi Mei, 2014, kuwa inaweza kukoleza mchakato wa amani kisiasa na kidini huko Mashariki ya kati.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, siku chache kabla ya kuanza maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi kwa Mwaka 2014 inayodumu takribani siku nane, alimwandikia Rabbi Riccardo di Segni, ujumbe wa matashi mema katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi.







All the contents on this site are copyrighted ©.