Maisha ni mchaka mchaka, vinginevyo utachakachuliwa!
Daima ni mchakamchaka. Tabia ya watu wa ulimwengu wa leo ni ile ya mchakamchaka. Kila
kitu kinaenda kwa kasi. Taarifa zinaenda kwa kasi kwa njia ya pembejeo za mawasiliano
ya haraka, barabara nzuri na za mikato, na wenzetu walioendelea ndiyo wana magarimoshi
yanayoenda kwa umeme kwa mwendo wa kasi.
Tuna kila kitu tunachokitaka kwa
haraka, daima tuko katika mchakamchaka na kiherehere cha kufanya mambo kama vile tuna
wasiwasi wa kutofika tunakotaka kufika au kutofanikiwa kufanya kwa wakati wake kile
tunachotaka kukifanya. Ama kweli ni mchakamchaka wa maisha. Mtu yupo katika kupiga
mbio za maendeleo katika maisha. Mtu anapiga mbio kwa vile hana uhakika wa kuwasili
au kufikia juu kijamii au kiuchumi au hata kuwazidi wengine. “Tukimbie wakati wengine
wanatembea!”
Hali hii ya mchakamchaka na ya mbiombio ndiyo unayoikuta katika
Injili ya leo. Mtakatifu Yohani anaposimulia kuhusu kaburi wazi lililokutwa asubuhi
ile ya ufufuko, anawaonesha wahusika wote wa tukio lile wakiwa katika mbiombio na
mchakamchaka: Maria Magdalena ndiye mwanakiherehere aliyefungia. Alikurupuka asubuhi
sana kungali bado giza kwenda kaburini. Alipolikuta jiwe lililofunika kaburi limeondolewa
hapo ndipo ilipoanza patashika ya mchakamchaka. Akaenda mbio kwa wanafunzi. Nao wale
wanafunzi Simon Petro na Yohane wakaanza mchakamchaka.
Tunaambiwa wakaondoka
mbio wote wawili kwenda kaburini. Yohane akamzidi mbio Petro akafika wa kwanza kaburini.
Kulikoni? Yaonekana mbio hizo zilipigwa kutokana na wasiwasi, na kiherehere cha kujua
kumetokea kitu gani. Budi ieleweke kwamba katika mazingira kama haya, binadamu anakuwa
amepagawa na kitu anachokuwa na uhakika nacho kwamba kinaweza kikatokea. Yaani, kinakuwa
ni kituko kipya kabisa anachotegemea kukiona au kukipata, kitu kitakachotokea au kilichoishatokea
kabla. Katika mantiki hiyo mtu huwa haweza kutulia au kujidanganya kutulia. Wasiwasi
na kiherehere chake ni kutaka kukiona au kukijua ni kitu gani ambacho ni budi kitokee
lakini hakijui.
Endapo kwa hawa wanafunzi wawili wangemwona Yesu kuwa si kitu
cha maana au si kitu cha kukijali, hapo tungewaona wametulia na kufanya mambo kitulivu.
Wangeenda kaburini kitulivu tena kwa ajili ya udadisi tu, siyo zaidi. Injili ya Yohani
inatafuta kutuingizia vionjo vya wanafunzi hawa wawili, Petro na Yohani wanaokimbia
kwenda kaburini. Nafikiri pengine, kwa wote wawili kuna woga labda kuna kitu siyo
kwamba hakikwenda sawa, bali wanaonja kwamba imani yao inalazimika kukua ili kutobaki
katika woga wa kumtamani tu Bwana wao aliyekufa na sasa hayuko tena. Mbio yao inadhihirisha
imani yao. Siyo imani kama ya yule aliye na uhakika bila wasiwasi, la hasha, vinginevyo
wangekuwa wamepoozwa, na kukosa mwelekeo na hivi kuchanganyikiwa na miguu kutetemea.
Wangekosa nguvu kabisa ya kukimbia, hivi daima wangekuwa wanajikwakwaa na kuanguka.
La hasha, kuna kitu!
Mbio na kiherehere cha Mkristu Mkristu ni yule anayekimbia,
anayepiga mbio katika maisha. Mbio za mkristu siyo zile zitokanazo na kutokuwa na
uhakika wa kuwasili au kufikia juu kijamii au kiuchumi au kupiga mbio za kuwazidi
wengine, bali anakimbia kwa vile anajisikia kuwa ni muhimu kuonja uwepo wa Mungu katika
maisha yake binafsi.
Tunajitambua katika mbio hizi? Tuna wasiwasi hata sisi
katika kumwelewa Kristu angalao kidogo Kristu ambaye wakati mwigine tunaamini amekufa
na kuzikwa katika maisha na katika maisha ya jamii?
Tunakubaliana na kupokea
hatari ya kuanguka na kujikwaa katika mwendo wetu wa imani? Tunasadiki kwamba kuwa
na imani kunamaanisha kwenda mbele katika kutafiti na kuhitaji kupanua uelewa wetu
wa imani. Au tunatafuta kwa mbinu na gharama zozote zile kutafuta au kubaki mahali
pamoja penye kutupatia uhakika na usalama? Kanisa (tuko wote humo ndani) wakati mwingine
hupunguza kasi, au mwendo na kutamani au kutulia katika uhakika na usalama wa hali
tuliyofikia.
Petro na Yohane, wakiwa wameambukizwa na kasi ya Magdalena wanaanza
kukimbia pamoja. Tuanze hata sisi mchakamchaka wa kumtafuta Yesu, tuwahusishe
katika mchakamchaka huo hata wale walio karibu nasi, labda wamezuiwa na matatizo fulani
au na harakati za maisha ya leo.
Heri sana kwa Pasaka yenye mbio… ili maisha
yasikwame.