2014-04-19 14:14:58

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaombea amani Barani Afrika


Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika ujumbe wake kwa Pasaka kwa Mwaka 2014 anawaalika Wakristo kutumia fursa ya Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka huu ili kuonesha ushuhuda wa umoja, mshikamano na upendo wa kidugu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka. Makanisa yote yanaadhimisha Siku kuu ya Pasaka, Jumapili tarehe 20 Aprili 2014.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, tukio la kuadhimisha kwa Siku kuu ya Pasaka kwa Makanisa yote kwa pamoja, linapaswa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa Makanisa yote, kama kielelezo na ushuhuda wa umoja kwa walimwengu ili wapate kuamini.

Hii ni changamoto kwa Makanisa kuhakikisha kwamba, yanaendeleza majadiliano ya Kiekumene, ili kuweza kuadhimisha Pasaka kwa pamoja. Maadhimisho ya Pasaka kwa tarehe tofauti ni kuendelea kutoa ushuhuda wa Kanisa lililogawanyika, kinyume kabisa cha kanuni ya imani inayofumbatwa kutoka katika mafundisho ya mitume! Mgawanyiko na mpasuko wa Makanisa ni mambo ambayo yanakwamisha mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa maisha.

Injili ya Kristo inapaswa kutangazwa na Wakristo wakiwa wameungana na kushikamana kama ndugu katika Kristo na kwa njia hii, Walimwengu wapate kumwamini Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika Kipindi hiki cha Pasaka linapenda kutolea sala na maombi yake kwa watu wenye mahitaji mbali mbali duniani, lakini kwa namna ya pekee: Syria na Mashariki ya Kati ambako watu wanaendelea kuteseka kutokana na vita pamoja na majanga asilia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasali kwa ajili ya kupata amani na utulivu huko Ukraini ambako kuna misigano ya kijamii: Sudan ya Kusini inayoendelea kuogelea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe; Nigeria ambayo imekumbwa na jinamizi la mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, bila ya kuwasahau wananchi kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambao kwa sasa wamechoshwa na vita na wanataka kweli amani na utulivu viweze kutawala kati ya watu!








All the contents on this site are copyrighted ©.